Featured

    Featured Posts

RC MNDEME AWAAGIZA WAKUU WA TAASISI ZA SERIKALI KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI KUANZIA NGAZI ZA CHINI

Na Albano Midelo, Ruvuma

Mkuu wa mkoa Ruvuma Chistina Mndeme  amewaagiza wakuu wa Taasisi zote za Serikalini mkoani hapa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuanzia ngazi za chini.

Mndeme ametoa agizo hilokauli katika kikao cha kazi cha watendaji na wakuu wote wa Taasisi za  serikali mkoani hapa kilichofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa Songea.

Amewata watendaji hao kusikiliza kero za wananchi kwa wakati na kuwaagiza kutosubiri kero kuwafikia ofisini badala yake waweke ratiba ya kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.

Mndeme ameagiza kila Halmashauri na Taasisi kuunda mkakati wake wa kushughulikia kero za wananchi ili kupunguza kero hizo kuanzia ngazi ya chini.

Sasa hivi tuna tatizo la mara kwa mara la kukatika kwa umeme,wewe Meneja wa TANESCO kazi yako ni nini, watu wamelipia umeme, hawajaunganishiwa umeme, wewe ukiwa ni Meneja wa TANESCO  kwanini huendi kwa wananchi na kutoa sababu za kero hizo, tutoe taarifa kwanini umeme umekatika, mpaka mimi Mkuu wa Mkoa ndiyo nikatoe taarifa kwa wananchi?" alisema Mndeme.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amezitaja sababu mbili kubwa zinaosababisha kero kwa wananchi ni kutokufanyika vikao vya kisheria na wananchi  na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri miongoni mwa watendaji wa serikali hivyo ameagiza kufanyika kwa vikao vya kisheria  na kuimarisha mahusiano ndani ya Taasisi za serikali ambayo yatasaidia kupunguza kero kwa wananchi.

Tukitekeleza majukumu yetu vizuri kwa wananchi, tutaifanya kazi ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa nyepesi, sisi ndiyo tupo chini, tutoke maofisini, tusisubiri ziara ya Mkuu wa Mkoa, ninyi wakuu wa Taasisi mnaruhusiwa kwenda kuzungumza na wananchi na kutatua kero zao, alisisitiza.

Mndeme ameagiza kila Taasisi kuandaa rejesta ya malalamiko ya ambayo itaratibu malalmiko pia kuunda timu ndogo itakayosaidia kuratibu malalamiko na kuyafikisha kwa mkuu wa Taasisi na kwamba kero za kisera zipelekwe ngazi ya juu ili ziweze kupata utatuzi wa kisera.

Ili kuhakikisha utatuzi wa kero unakuwa endelevu, Mkuu wa Mkoa ameziagiza Taasisi za serikali kila mwisho wa mwezi kufanya tathimini namna kero zilivyoshughulikiwa na kutoa taarifa za kero zinazohitaji ufafanuzi wa kisera kwa wananchi.


"Nimekuwa nikipokea kero mbalimbali ambazo wakati mwingine kero hizo zingetatuliwa katika ngazi ya wilaya au kijiji, sasa nimeona ni vema niwaite wakuu wa Taasisi zote, kwa sababu tunapaswa kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yetu", alisema Mndeme.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Ruvuma  Oddo Mwisho amesema ilani ya CCM ya 2020/ 2025 inalitaja moja ya jukumu lake ni kusikiliza malalamiko ya wananchi hivyo jambo linalofanywa na uongozi wa mkoa  wa Ruvuma ni utekelezaji wa ilani. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema katika kushughulikia malalamiko ya wananchi na kwamba hakuna mfumo wa pamoja, hali inayosababisha wananchi kutojua wakimbilie wapi katika kupata suluhu ya matatizo yao.

Ili kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Mkoa wa Ruvuma umeazimia kuunda timu ya Mkoa ya kutatua kero zinazowakabili wananchi ambayo itakutana kila baada ya miezi mitatu.

*******

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alizungumza na wakuu wa Taasisi zote za serikali na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nne mkoani humo katika Kikao kazi cha kuzungumzia utatuzi wa kero za wananchi kuanzia ngazi ya chini kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Baadhi ya wakuu wa Taasisi za Serikali na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma wakiwa katika kikao kazi kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea, jana.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana