Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa maarufu kama Baraza la 75 limekamilisha mkutano wake maalum uliolenga kumkumbuka na kumuenzi Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 na kuzikwa Machi 26.
Baraza limechukua hatua hiyo kutambua mchango wa Dk Magufuli aliyekuwa kiongozi wa nchi mwanachama miongoni mwa nchi 193 wanachama wa Baraza hilo la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Baraza, Katibu Mkuu na wenyeviti wa makundi matano yanayounda Baraza ambayo ni Afrika, Asia na Pasific, Ulaya Mashariki, Ulaya Mshariki, Amerika ya Kusini na Karibea kushiriki mkutano huo akiwemo mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN) Balozi Profesa Kennedy Gastorn jijini New York, Marekani.
Akihutubia mkutano katika kumuenzi Hayati Magufuli, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres amesema, katika kumkumbuka kiongozi, UN itaenzi jitihada zake za kusimamia upatikanaji wa huduma za kijamii na mapambano dhidi ya rushwa.
Ameongeza kuwa aliyekuwa rais hayati Magufuli alijijengea umaarufu katika maendeleo ya miundombinu na viwanda ambayo ni dhana muhimu katika kukuza uchumi sambamba na kufanikisha nchi yake kuingia kwenye nchi zenye uchumi wa kati kabla ya kipindi cha makisio cha mwaka 2025.
Aidha akiendelea kutoa sifa za kiongozi huyo aliyedumu kwa miaka mitano na miezi michache madarakani, Guterres amesema, hayati Magufuli aliwezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wapya kujiunga na shule za sekondari sambamba na kuboresha uwezo wa upatikanaji wa nishati ya umeme nchi nzima.
"Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, kwa mara nyingine tena ninapenda kutoa pole kwa familia ya Rais, Serikali na Watanzania kwa jumla. Tunatambua historia ya ushirikiano uliotolewa kimataifa na kikanda, na ninachukua nafasi hii kusisitiza na kurudia tena kusema Umoja wa Mataifa tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan na tunasimama na wananchi wa Tanzania katika kuendeleza na kusaidia mafanikio ya kimaendeleo kwa Watanzania wote.
Post a Comment