Featured

    Featured Posts

WATAALAMU WA AFYA MUHIMBILI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA MAGONJWA YA DAMU

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Godwin Mollel akizungumza katika mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Himofilia ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka. Siku hiyo imeadhimishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Baadhi ya wagonjwa wa Himofilia na Selimundu wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Ugonjwa wa Himofilia duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akieleza umuhimu wa huduma ya afya kwa wagonjwa wa Himofilia.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaura akiwasilisha mada kwa wagonjwa wa himofilia wakiwamo watoto.
Edson mwenye Himofilia akimlisha keki Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel. Leo ni siku ya kuzaliwa kwa Edson ambaye amesherekea siku hiyo na watoto wenzake pamoja na wazazi.

SERIKALI imewataka wataalamu wa afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoa elimu ya magonjwa ya damu nchini ikiwemo Himofilia ili wenye ugonjwa huo waweze kugunduliwa na kupelekwa mapema hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Wototo, Dkt. Godwin Mollel wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Himofilia ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka lengo ikiwa ni kuwaleta pamoja watu wenye matatizo ya Himofilia duniani.

Dkt. Mollel amesema wananchi wakipatiwa elimu ya ugonjwa huo itawasaidia kupunguza madhara na vifo vitokanavyo na magonjwa yasioambukiza ikiwemo Himofilia na Selimundu.

Naibu Waziri alimuagiza Mratibu wa Mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu Wenye Magonjwa ya Damu,’ kwenda katika hospitali za rufaa, kanda na wilaya ili kutoa elimu ya ugonjwa huo ambayo itawasaidia watu wenye Himofilia kufika hospitali mapema.

“Dkt. Stella hakikisha unakwenda katika hospitali za kanda kutoa elimu hii, nafikiri itakuwa njia rahisi kuwafikia wataalamu wengi wa afya nchini,” amesema Dkt. Mollel

Amesema maisha ya watu wenye tatizo la Himofilia yanahitaji uangalizi mkubwa ili kuzuia uvujaji damu, ulemavu na vifo, hivyo hulazimika kupimwa ili kubaini aina ya Himofilia inayo msumbua mgonjwa na kupata matibabu ya kuchomwa factor (chembechembe za protini zilizokosekana mwilini) ili kusaidia kugandisha damu.

“Kama tunavyofahamu, Himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda ambao unasababishwa na   ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu, hivyo husababisha damu kuvuja muda mrefu baada ya mgonjwa kupata jeraha na kuhatarisha maisha,’’ amesema Dkt. Mollel.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel alishiriki kwenye maandamo ya kuadhimisha siku ya ugonjwa wa Himofilia duniani na alizindua dawa mpya ya Emicizumab ambapo Waziri alishuhudia mmoja wa wagonjwa wenye Himofilia akichomwa sindano Emicizumab.

Pia, Waziri alizindua gari la mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu wenye Magonjwa ya Damu.’

Naye Mkurugezi Mtendaji wa Hospitalli ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema mwaka jana Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zilizochaguliwa kupewa msaada wa dawa mpya ya Emicizumab kwa ajili ya wagonjwa wa Himofilia

“Mhe. Waziri, ninafurahi kukwambia kuwa Tanzania tumekuwa nchi ya nne barani Afrika kupokea msaada wa dawa hizi na kuanza kuitumia rasmi ambapo kwa Afrika Mashariki, Tanzania inakuwa nchi ya pili baada ya Kenya na nyingine zilizopokea dawa hizi barani Afrika ni pamoja na Zambia na Cameroon”.

“Dawa hizi ni ghali sana hivyo kwa kuwa mradi huu ni wa miaka mitatu tunaomba Serikali ione namna ambavyo itaendeleza huduma hii iweze kuwa endelevu baada ya mradi kuisha muda wake,” amesema Prof. Museru.

Mmoja wa wanachama wa chama cha watu wenye magonjwa ya Himofilia, Bi. Regina Shirima aliitaka jamii hasa kinababa kushirikiana na kinamama katika kuwapeleka hospitali watoto wenye himofilia kwani baadhi ya kina baba wamekuwa wakiwakimbia wake zao baada ya kubaini mmoja ya watoto ana tatizo la Himofilia.

“Tunawashukuru wataalamu wa MNH akiwamo Dkt. Stella, tunawapigia simu usiku mara mtoto anapovuja damu,” amesema Bi. Shirima.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ikishirikiana na wadau wa afya Novo Nordisk Foundation (NNF) na Novo Nordisk Hemophilia Foundation (NNHF), ilianzisha mradi huu ili kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Kenya.

Takwimu za kidunia zinaonyesha mtu mmoja kati ya watu 10,000 ana tatizo la Himofilia. Mpaka sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 56 mpaka 60 hivyo inaweza kuwa na wagonjwa wapatao 6,000 hadi 12,000.  Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 97 ya watu wenye ugonjwa huu duniani bado hawajagundulika ambapo kwa upande wa Tanzania waliotambulika na wanaendelea na matibabu ni 167 tu.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana