Kamati ya maalumu ya uchunguzi ya Mahakama ya Mawaziri ya serikali ya Kuwait imetoa amri ya kupandishwa kizimbani Jabir al Mubarak, Waziri Mkuu wa zamani na Khalid al Jarrah, waziri wa zamani wa ulinzi pamoja na viongozi wengine wanne wa nchi hiyo, kwa tuhuma za ufisadi na wizi wa fedha.
Kwa mujibu wa kamati hiyo ya uchunguzi ya mahakama maalumu ya mawaziri ya serikali ya Kuwait, moja ya kesi zinazowakabili watuhumiwa hao ni ufisadi wa mamia ya mamilioni ya dola katika mkataba mmoja. Kamati hiyo imejiridhisha kuwa watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu katika ufisadi huo.
Kikao cha kwanza cha kusikiliza kesi ya Waziri Mkuu wa zamani, Waziri wa Ulinzi wa zamani na viongozi wengine wanne wa Kuwait, kitafanyika Jumanne ijayo.
Hivi karibuni Mahakama ya Mawaziri ya serikali ya Kuwait ilimpiga marufuku Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Jabir al Mubarak kutoka nje ya nchi baada ya kumsaili kuhusu kesi inayojulikana kwa jina la Makosa ya Fedha ya Mfuko wa Jeshi.
Jabir al Mubarak alikuwa Waziri Mkuu wa Kuwait kuanzia mwishoni mwa mwaka 2011 hadi mwishoni mwa mwaka 2019. Alilazimika kujiuzulu baada ya kufichuliwa ufisadi mkubwa katika mfuko wa jeshi la nchi hiyo.
Amir wa Kuwait, Nawaf Al‑Ahmad Al‑Jaber Al‑Sabah amehimiza kufuatiliwa kwa kina kesi hiyo na sheria kufuata mkondo wake, kwani ndivyo wanavyohimiza wananchi wa nchi hiyo.
Post a Comment