Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Francis Masanja akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Richard Francis Sanga leo jijini Dodoma ambapo amesema serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kutangaza vivutio vyote vya utalii nchini pamoja na kurekebisha miundombinu ya maeneo ya uhifadhi ili kurahisisha ufikaji wa Watalii katika maeneo hayo.
********************
Wizara ya Malisili na Utalii imesema mikakati yake iliyo nayo kwa sasa ni kuzitangaza Hifadhi zote za Taifa ndani na nje ya nchi ikiwemo Hifadhi ya Kitulo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga lililokuwa likihoji upi mkakati wa serikali wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ili ifahamike kwa watalii ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Mhe.Masanja amesema Hifadhi ya Kitulo ni moja kati ya Hifadhi yenye sifa ya kipekee kwa kuwa na jamii mbalimbali za maua (Serengeti of Flowers) na kwa kutambua hilo Serikali imekuwa ikiendelea kuitangaza.
Akijibu swali hilo Mhe. Masanja amesema miongoni mwa mikakati ya kuitangaza Hifadhi hiyo njia mbalimbali zimekuwa zikitumika kama ilivyo katika Hifadhi nyingine ikiwemo kupitia tovuti na mitandao ya kijamii pamoja na kuandaa video na filamu mbalimbali.
Aidha, Amesema ili kuvutia Watalii wengi zaidi Serikali imekuwa ikiimarisha miundombinu ya barabara ndani ya Hifadhi hiyo kwa lengo la kurahisisha ufikikaji wa maeneo ya vivutio vya Utalii.
‘’ Tumeanzisha Chaneli maalumu ya utalii ya “Tanzania Safari Chanel” pamoja na kujenga sehemu ya malazi ya bei nafuu ili kuwavutia Watalii wengi kutembelea Vivutio vya Utalii nchini, amesisitiza Naibu Waziri Masanja.
Akijibu maswali ya nyongeza kuhusiana na Uwekezaji katika maeneo ya Hifadhi, Mhe. Masanja amesema Wizara ya Maliasili na Utalii haina gharama yeyote inayohusiana na uwekezaji, Hivyo amewatoa wito kwa Wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo ya Hifadhi zilizopo
Katika hatua nyingine, Mhe Masanja amesema serikali imejipanga kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhakikisha inaimarisha Miundombinu katika maeneo yote ya Hifadhi kwa kutenga fedha ya kutosha ili kuwavutia Watalii kutembelea maeneo ya Hifadhi.
Ameongeza kuwa katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imezingatia masuala ya utangazaji wa vivutio vya utalii pamoja na kuboresha miundombinu ikiwemo barabara,viwanja vya ndege na maeneo ya malazi kwa wageni ili kuvutia watalii kutembelea maeneo hayo kwa urahisi.
Post a Comment