Featured

    Featured Posts

PONGEZI KWA RAIS MHE.SAMIA SULUHU KWA KUTOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 5,000

 

************************************

ITAKUMBUKWA kuwa Aprili 26, 2021 siku ya Maadhimisho ya Miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza msamaha kwa wafungwa 5,001 waliokuwa wakikabiliwa na adhabu ya vifungo mbalimbali.

Kufuatia uamuzi huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake huo kwa wananchi anaowaongoza.

Tume inachukulia uamuzi huo wa Rais kama jambo ambalo linaweka nguvu na mkazo katika sehemu ya majukumu yake ya kuhakikisha haki za binadamu zinafurahiwa na watu wote ikiwemo wale walio magerezani. Aidha, Tume imefurahishwa na inaunga mkono kauli aliyoitoa Mhe. Rais ya kuwataka wafungwa walioachiwa huru kutumia vyema mafunzo waliyoyapata wakiwa gerezani na waungane na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa huku wakiheshimu na kuzingatia sheria.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 25(1) (a), na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 22(1) (a) kila mtu anao wajibu wa kushiriki katika kazi halali ya uzalishaji mali.

Wakati huo huo Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 23(1) ya Katiba ya Zanzibar zinatoa wajibu kwa kila raia kutii sheria za nchi. Ni matumaini ya Tume kuwa wafungwa walioachiwa huru na wananchi wote kwa ujumla watazingati wito huu wa Mheshimiwa Rais kwa manufaa ya taifa letu.

Mwisho, Tume inatoa ushauri kwa jamii na wanufaika wa msamaha wa Mheshimiwa Rais kama ifuatavyo:

  1. Wafungwa walioachiwa huru wakayatumie vyema mafunzo na maarifa waliyoyapata wakiwa gerezani kufanya kazi za uzalishaji mali na kujipatia kipato. Pia wale waliopunguziwa adhabu zao wawe na mwenendo mzuri ili hatimaye nao waweze kuachiwa huru. Tume inaamini wakifanya hivyo ndio njia pekee ya kumpa faraja Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake.

  1. Tume inawasihi Watanzania wote kuwapokea ndugu zao hawa kwa mtazamo chanya na kushirikiana nao katika kazi za ujenzi wa taifa, kwani kinyume na hapo, wakiwatenga itawajengea picha ya kuona wananyanyapaliwa na hivyo kupelekea uwezekano wa kurudia makosa yatakayowarudisha tena gerezani.

  1. Tume inawaasa wanufaika kuwa raia wema na kutotenda makosa tena.

Tume inapenda kuchukua nafasi hii pia kuuhakikishia umma wa Watanzania kuwa itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuelimisha wananchi kuhusu masuala yote ya haki za binadamu na utawala bora ili maendeleo na amani vizidi kushamiri nchini.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana