Ikulu, Dar es Salaam
Rais Samia Suluhu Hassan amemsimamisha kazi Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya leo, Alhamisi, Mei 13, 2021, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yake.
Taarifa ya Ikulu imesema, wakati huo huo, Rais Samia amemteua viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;
Rais amemteua Nsubili Akomeligwe Kajela Joshua kuwa Karani wa Baraza la Mawaziri na kabla ya uteuzi huu Joshua alikuwa akikaimu nafasi hiyo, huku akimteua pia Ayub Musa Makoye kuwa Naibu Karani wa Baraza la Mawaziri ambaye naye alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Rais Samia amemteua Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dk. Stergomena Tax kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute).
Pia Rais Samia amemteua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dk. Laurian Ndumbaro kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Uongozi Insitute.
Sambamba na uteuzi huo, Rais Samia amefanya uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi ambao ni Balozi Riitta Swan, Prof. Penina Mlama, Lina Soiri, David Walker, Suzan Mlawi, Dk. Hamis Mwinyimvua na Prof. Samwel Wangwe na Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo tarehe 13 Mei, 2021.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Ishmael Andulile Kasekwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na uteuzi huo ulianza Mei 10, 2021 kuchukua nafasi ya Dk. Rosebud Kurwijila ambaye amemaliza muda wake.
Post a Comment