Featured

    Featured Posts

WIZARA YA AFYA YAANZA UTEKELEZAJI WA MABORESHO YA HUDUMA ZA MATIBABU KWA WAZEE

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kuangalia Hali ya utoaji huduma kwa Wazee kwenye hospitali hiyo

#Tunaboresha Afya

#KaziIendelee 



Na.WAMJW-Dodoma


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya ufuatiliaji  wa maelekezo yake  katika kuboresha huduma za matibabu kwa wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kujionea jinsi walivyoweza kutekeleza maagizo ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee wanaofika kupata matibabu hospitalini hapo.


Dkt. Gwajima amesema mahitaji ya maboresho ni mengi  hivyo wizara yake imeona ianze na vitu  vile vya msingi  ambavyo wazee wamekuwa wakiyalalamikia   kila siku wanapofika kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya.


Ametaja malalamiko yanayokuwa yakilalamikiwa na wazee  wanapofika kwenye vituo vya afya ni pamoja na mapokezi yasiyoeleweka na kutokupata huduma iliyokusudiwa na kuongeza kuwa   wazee nguvu zimekwisha hivyo wanahitaji kuongozwa kwahiyo wizara yake wamefanya maboresho kwa kuwa na watu maalumu wa kuwapokea wazee hao pale wanapoifika hadi kuondoka na kuwatambulisha kwa kuvaa sare maalumu.


“Kila kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare ambayo itamtambulisha na imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’  pamoja na kuweka mabango yanayomuelekeza au kumuongoza mzee wapi atapata huduma anazozihitaji na ambayo yameandikwa "Mpishe Mzee apate huduma kwanza".


Dkt. Gwajima amesema maelekezo hayo wameyatoa katika hospitali na vituo vya afya vyote na kwa hatua hiyo sasa wizara inaenda kutengeneza muongozo ambao utakua wa uwiano kwa hospitali zote.  Hata hivyo ameipongeza hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma kwa kuanza utekelezaji huo na kuwa itakuwa ya mfano wengine kujifunza utaratibu unaotumika na kuboresha kulingana na mazingira yao.


Aidha, Dkt. Gwajima amewataka hospitali zingine kutokusubiri miongozo katika kutekeleza  maelekezo yanayolewa na kusiwe na visingizio vingi kwamba haiwezekani kwani maagizo yanayotolewa yanawezekana na utekelezaji wake ni wa mara moja hususan katika hospitali za kuanzia halmashauri hadi ngazi ya Taifa.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vivian Wonanji  amesema idara yake imeandaa mkakati wa huduma wa wazee wa  miaka kumi na ifikapo mwezi Juni mwaka huu wataanza kuandaa mpango wa utekelezaji wake.


Dkt. Wonanji amesema mpango mkakati huo utakuwa na mambo makuu yakiwemo kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za wazee,"kama tunavyofahamu wazee wanahitaji mambo mengi ikiwemo masuala ya lishe na utengamao hivyo mkakati huo utakua na maono muhimu ambayo yatasaidia kuboresha huduma za wazee nchini”.


Wakati huo huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema hospitali yake imejipanga kuwahudumia wazee wa rika tofauti wakiwemo wenye uoni hafifu na hivyo waratibu wa wazee huwafuata wazee mara wafikapo hospitalini  hivyo wanashukuru mapokeo ya wazee pamoja na wagonjwa wanaofika kupata huduma. 


Mnamo tarehe 7 Mei, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dar es salaam aliahidi kuboresha tiba kwa wazee  kwani tiba ni haki yao ya msingi  katika daraja lolote lile watakalokua wanaugua kuanzia vituo vya afya, zahanati hata hospitali za Taifa.





author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana