Na John Walter-Babati.
Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru mkoa wa Manyara mwaka 2021 zimeendelea kuzindua,kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi katika wilaya za mkoa huo.
Katika Miradi ya Maendeleo ya wananchi wilaya ya Babati imehusisha michango yao ya jumla ya shilingi Milioni 20,600,000, wadau wengine milioni 306,409,269, Halmashauri Milioni 119,474,000 na serikali kuu Bilioni 2,302,602,264.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi katika wilayani Babati amezindua mradi wa Vijana wa Pikipiki mtaa wa Miomboni Halmashauri ya mji wa Babati ikiwa ni asilimia nne ya mkopo kwa vijana kutoka Halmashauri ambapo Takribani pikipiki thelathini zilizokabidhiwa kwa vijana hao zimegharimu shilingi milioni 98,880,000.
Mbio za Mwenge zimeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Mabweni shule ya Sekondari Ayalagaya halmashauri ya wilaya ya Babati ambao thamani yake shilingi Milioni 311,409,269 fedha kutoka kwa mfadhili Kareem Foundation huku wananchi wakichangia shilingi Milioni 5,000,000.
Katika Kijiji cha Imbilili halmashauri ya mji wa Babati mwenge ulitembelea na kuona mradi wa maji ambao umekamilika kwa fedha za serikali kuu shilingi Milioni 356,118,995.Aidha kiongozi wa Mbio za Mwenge alitembelea na kuona mradi wa TEHAMA unavyofanya kazi katika kituo cha afya Magugu halmashauri ya wilaya ya Babati wenye thamani ya shilingi Milioni 14,400,000.
Pia Mwenge uliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Babati ambao unaendelea katika hatua mbalimbali za ujenzi ambao unahusisha michango ya wananchi shilingi milioni 15,600,000 na serikali kuu Bilioni 1,500,000,000 ambayo inafanya jumla kuwa shilingi bilioni 1,521,794,000.
Mbio za Mwenge ambazo hutoa ujumbe mbalimbali kwa wananchi katika maeneo unapopita ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Luteni Josephine Mwambashi, aliwataka Wazazi na walezi Nchini kuhakikisha wanatumia vyakula lishe ili kujenga mwili na akili kwa Watoto wao.
Mwambashi alisema Mbio za Mwenge zinaendelea kusisitiza kuhusu matumizi sahihi ya lishe bora ambapo alieleza lishe bora kwa watoto ni jukumu la kila mzazi na ni haki ya kila mtoto kuipata ili akue kimwili na kiakili ni lazima wapate lishe bora ambayo itawasaidia kuwa vijana shupavu na nguvu kazi ya Taifa .
Pia amesisitiza Wajawazito kufika katika vituo vya afya ili waweze kuwapatiwa elimu inayotolewa kuhusu uandaji wa lishe bora na Sahihi kwa mtoto ."Lishe bora si lazima ulaji wa chakula kingi bali lishe bora ni ulaji wa vyakula mchanganyiko vya lishe ikiwemo matunda,mbogamboga,"Alisisitiza Mwambashi.
Hata hivyo Kiongozi huyo alieleza Mbio za Mwenge pia zinaendelea kusisitiza mapambano dhidi ya malaria chini ya kauli mbiu isemayo ziro malaria inaanza na Mimi na chukua hatua kuitokomeza.
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange aliupokea Mwenge huo ukiwa Salama juni 13 kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Kiteto Kanali Patrick Songea na ameukabidhi kwa mkuu wa wilaya ya Hanang Gharib Lingo ukiwa salama.
Risala ya Utii iliyosomwa na Katibu tawala wilaya ya Babati Hassan Matipula ulibainisha mambo mablimbali yanayofanywa katika wilaya kudhibiti utumiaji wa madawa ya kulevya na kupiga vitendo vya rushwa.Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 utakamilisha mbio zake katika wilaya ya Mbulu Juni kumi na tano ambapo mkuu wa wilaya hiyo Dr. Chelestino Mofuga ataukabidhi katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Ikumbukwe kuwa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 zilizinduliwa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdul katika Mkoa wa Kusini Unguja visiwani Zanzibar mahali alipozaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na zitahitimishwa mkoani Geita wilaya ya Chato mahali alipozaliwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya tano Oktoba 14, 2021.
Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu umebeba kauli mbiu isemayo ‘TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu itumike kwa usahihi na uwajibikaji”.
Post a Comment