Featured

    Featured Posts

SERIKALI KUPINGA VIKALI UKATILI DHIDI YA WAZEE

 
    Na Mwandishi Wetu,

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Doroth Gwajima amesema kuwa Serikali inakemea vikali na kupinga vitendo vya Ukatili dhidi ya wazee.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo  Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi Wazee yanayoadhimishwa Juni 15 kila mwaka.

Waziri Dkt Gwajima amesema kwamba Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee huadhimishwa ikiwa na lengo la Kulinda haki, Ulinzi na Usalama wa Wazee kama ilivyodhamiriwa kwenye azimio la Umoja wa kimataifa la mwaka 2011.

Dkt. Gwajima amesema Serikali inaendelea kutekeleza afua mbalimbali za kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wote hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa  Mkakati wa Kitaifa  wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee 2018/19 – 2022/23.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wasiojiweza na ambao hawana watu wa kuwatunza, Serikali inasimamia matunzo katika makazi ya wazee 13 yenye jumla ya wahudumiwa 262 (Me 163, Ke 100) na kuratibu huduma katika makazi 20 ya Taasisi za dini na watu binafsi yenye wahudumiwa 537 (Me 242, Ke 295) ambapo wazee hawa hupata huduma za chakula, malazi, mavazi, matibabu na msaada wa kisaikolojia na kijamii. 

Dkt.Gwajima amesema kuwa Serikali imeendelea kuwatambua na kuwapatia familia masikini wakiwemo wazee na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambapo hadi kufikia Septemba 2019, jumla ya Wazee 680,056 (Wanaume 258,674 na Wanawake 421,382) wamenufaika na mpango huo

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali inatambua kuwa wazee ni hazina ya taifa kutokana na ujuzi na uzoefu walio nao katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na katika kuhakikisha kuwa hazina hii inatumika ipasavyo, Serikali imeendelea na uundaji wa mabaraza ya wazee kote nchini. Jumla ya mabaraza 14,883 yameundwa kuanzia ngazi ya Vijiji/Mitaa, Kata, Wilaya na mikoa nchini.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mabaraza ya wazee yanaundwa katika ngazi zote ili wazee washirikishwe  ipasavyo katika maendeleo ya Taifa” alisema Dkt. Gwajima

Pia Waziir Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kuhamasika katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wote nchini. "

Tutumie siku hii katika kutafakari changamoto mbalimbali zinazowakumba wazee hapa nchini na kushirikiana kwa pamoja katika kuzitatua kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyoelekeza". Alisisitiza Dkt. Gwajima.

Tarehe 15 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee na kwa mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee inaongozwa kwa kauli Mbiu isemayoTUPAZE SAUTI KUPINGA UKATILI DHIDI YA WAZEE.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana