Napenda kuungana na Mamilioni ya Watanzania kusherehekea maadhimisho ya siku 100 tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan ale kiapo Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni siku zilizojaa maajabu, matumaini na mwangaza kwa Taifa letu.
Nitagusia baadhi ya mambo muhimu yaliyojili ndani ya siku 100 za Rais Samia Ikulu.
1. Rais Samia ameonyesha uhodari wa kupokea kijiti kwa kuendeleza yote mazuri na kuhakikisha anayakamilisha. Umahiri kwenye uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama vile uendelezaji ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ujenzi bwawa la umeme la Mwl. Nyerere nk. Karibia kote ametoa fedha na kazi inaendelea.
2. Rais Samia amesimamia mahusiano ya kidiplomasia kwa Tanzania na nchi jirani na kimataifa yanazidi kuimarika vilivyo. Mathalani kuimarika kwa mahusiano baina ya Tanzania na Kenya kutokana na pande zote kuondoa vikwazo vidogo vidogo vilivyokuwepo.
3. Rais Samia amefanikiwa kupandisha mishahara kwa kuondoa PAYE, kupandisha madaraja Watumishi, kulipa madai ya Watumishi ambayo hayakuweza kufanyika kwa miaka mingi lakini yamewezekana ndani ya siku 100 za utawala wake. Hakika Rais Samia ameupiga mwingi sana.
4. Rais Samia ameendelea kuwa mtetezi wa Wajasiliamali wadogo na hakusita kuonyesha makali yake kwa yeyote yule aliyewazingua. Hakika bodaboda, Mama lishe, Wamachinga na Wajasiliamali wote wadogo wanapewa heshima ya juu na Serikali ya Rais Samia kwa kulindwa vilivyo wasisumbuliwe na Mamlaka za Mapato, viongozi Serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama.
5. Rais Samia ameendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini na kufanya wawekezaji kukiri hadharani utofauti na maboresho ya kibiashara nchini. Mfano hai wa Mwekezaji ni Dangote ambaye ni Mwekezaji wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza saruji nchini, ameridhishwa na mazingira ya sasa kuwa hayana urasimu na milango ya biashara yamefunguka sana na yupo tayari kuongeza uwekezaji wa kiwanda kingine kikubwa Tanzania.
6. Rais Samia ametoa maelekezo ya yameshatekelezwa ya kufungua akaunti za Wafanyabiashara zilizofungwa kwa sababu mbalimbali na TRA na wakae meza moja na Wafanyabiashara kuona namna bora kumaliza changamoto zilizopelekea akaunti zao kufungwa. Hii imepeleka furaha na vicheko kwa Wafanyabiashara kote nchini.
7.. Rais Samia ameendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo wanaotuhumiwa na vitendo hivyo amekuwa akiwaweka pembeni na kutoa maelekezo uchunguzi ufanyike. Tumejionea hayo kule bandari, hazina nk.
8. Rais Samia ameendeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati kwa mwendo na kasi ile ile ya awali. Tunajionea miradi ya SGR, Bwawa la Nyerere nk ikiendelea kwa kasi ya ajabu. Huku ni kuenzi kwa vitendo na picha isiyo na shaka ya kuwa kitu kimoja.
9. Rais Samia ameongeza kasi ya ukuzaji ufanyaji biashara nje ya mipaka ya Tanzania. Mfano hai ni furaha na vicheko vya Wafanyabiashara wa Mahindi kwenda nchini Kenya kwa ulaini kabisa kufanya biashara.
10. Rais Samia ameendelea kuhakikisha anaimalisha ulinzi na usalama ndani na nje ya mipaka pamoja na kupambana vikali na madawa ya kulevya. Kukamatwa kwa zaidi ya tani ya Madawa ya kulevya kule mkoani Lindi; Mauaji ya Maalbino hayapo; Matukio ya wizi na ujambazi yamepungua kwani walianza kumbipu wakakutana na shoo kali ya Rais Samia. Pongezi za kipekee kwa vikosi vyote vya ulinzi na usalama nchini kwa kazi kubwa wanazoendelea kuzifanya kila siku.
11. Ilani ya uchaguzi 2020 - 2025 inaendelea kutekelezwa vyema kwa vitendo kwa kasi kubwa; Shughuli za Serikali zinaendelea kufanyika pasipo mkwamo wowote ule. Huu ni ushahidi wa kazi kubwa ya ukusanyaji imara wa kodi unaopelekea upatikanaji wa mapato ya ndani yanayowezesha nchi kujitegemea kiuchumi.
12. Ndani ya siku 100 tumeshuhudia ajira zikitangazwa na Watu kuajiriwa kwenye sekta za afya, elimu, ulinzi na utawala.
13. Ni Rais Samia huyu huyu ameonyesha kujali zao la Korosho kwa kuondoa makato ya Tsh. 110 ya pembejeo; Kuteua Mwenyekiti Bodi ya Korosho ambaye hakuwepo kwa zaidi ya miaka 4; Kuagiza bandari ya Mtwara ianze kusafirisha Korosho pamoja na kuto agizo kwa Mamlaka ya bandari Mtwara kuondoa tozo zote zinazowakwaza Wasafirishaji.
14. Rais Samia ameonyesha imani kubwa kwa Vijana kuwapa nafasi za kiuongozi. Vijana ambao ndio nguvu kazi na idadi kubwa ya Watu nchini wameonyesha furaha, imani na ushirikiano mkubwa kwake.
15. Rais Samia ameagiza uunganishwaji wa umeme uwe Tsh. 27,000/= mijini na vijijini. Hivyo tangu Rais Samia awe Ikulu kuunganishwa umeme nchi nzima ni Tsh. 27,000/=
Itaendelea
Shilatu, E.J
Post a Comment