Na Mwandishi Maalum, Morogoro
Wananchi katika Kata ya Kingolwira na Bigwa mkoani Morogoro, wameamua kujielekeza katika Shughuli za Ufugaji wa Nyuki na kuachana na kazi ya Ukataji miti hovyo na Uchomaji mkaa ili kulinda na kuhifadhi Mazingira hususani kwenye Chanzo cha Maji katika Bonde Dogo la Mto Mgolole.
Bonde Dogo la Mto Mgolole ni miongoni mwa vyanzo vya maji, ambavyo awali vilikuwa hatarini kuharibiwa kwa sababu ya kuingiliwa na Shughuli za Kibinadamu.
Kufuatia hali hiyo Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, imeamua kuiwezesha Jumuiya ya Watumia maji Mgolole kufanya Shughuli za Ufugaji Nyuki kwa kuipatia mizinga, ikiwa ni hatua mbadala ya kuwaingizia Kipato Wananchi wa kata za Kingolwira na Bingwa.
Afisa Mkuu wa maendeleo ya Jamii wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Halima Faraji amesema Jumuiya ya Watumia maji Mgolole, imeipa kisogo Shughuli ya Ukataji miti hovyo, Uchomaji mkaa na ufyatuaji tofali ili kulinda mazingira hususani kwenye chanzo hicho cha maji.
"Kwa hiyo Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu, imeona mwitikio mkubwa wa Wananchi, Sasa wanaelewa Sheria na taratibu zinazo simamia Suala la utunzaji na uhifadhi wa Rasilimali maji" alisema Halima Faraji.
Baadhi ya Wananchi katika Kata hizo mbili akiwemo Kobelo Kobelo na Pepetua Kessy, wamesema Suala la Ufugaji nyuki limekuwa na tija kwao, kwa sababu licha ya kupata kipato cha Kujikimu lakini Wameweza Kulinda mazingira na Kuhifadhi Chanzo cha maji Katika Bonde hilo Dogo la Mto Mgolole.
“Tutakuwa wanyimi wa Fadhila, tusipotoa Shukrani zetu kwa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, kwa kutuwezesha kuwa wafugaji wa nyuki kwa Sababu tumepata faida kubwa na uelewa wa kutosha kuhusu mazingira, na kama Jamii tunapaswa kulinda Rasilimali maji na Mazingira” Walieleza Wananchi hao.
Ili kulinda Mazingira hususani vyanzo vya maji, Siku ya Mazingira Duniani iliyoadhimishwa June 5 mwaka huu, ililenga kuhamasisha Jamii kutumia nishati mbadala ili kuongoa mifumo Ikiolojia.
Baadhi ya Mizinga ya nyuki ambayo imekabidhiwa kwa Jumuiya ya Watumia Maji Katika Bonde Dogo la Mto Mgolole, ikiwa ni mbadala wa kufanya Shughuli zisizoharibu Mazingira kwa lengo la Kutunza na Kuhifadhi chanzo hicho cha maji.
Post a Comment