Na Karama Kenyenko,Michuzi TV
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia kwa dhamana aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kulthum Mansoor (57) aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi baada ya kufutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha.
Akisomewa masharti ya dhamana mshitakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho vya Taifa au vitambulisho vinavyotambulika watakaosaini bondi ya Sh. milioni 20.
Mansoor ametimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili.
Akisoma mashtaka mapya, Wakili wa Serikali Sylvia Mitanto alidai kati ya Januari 2013 na Mei mwaka 2018 akiwa mtumishi wa Takukuru alighushi barua ya Agosti 13,2003 kwa lengo la kuonesha imetolewa na Halmashauri ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Inadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017 akiwa eneo la Upanga mshtakiwa Kuluthum alijipatia Sh milioni 5.2 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Francis Mavika kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua siyo kweli.
Katika shtaka la tatu imedaiwa tarehe tofauti tofauti katika eneo la Upanga mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh milioni tatu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Wakati Katondo kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.
Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kujipatia Sh.milioni tano kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Gogo Migutah, huku akijifanya kuwa anamiliki kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo wakati akijua ni uongo.
Pia anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh milioni saba kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Ekwabi Majungu kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.
Inadaiwa tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh milioni saba kutoka kwa mtumishi wa Takukuru,John Sangwa kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.
Katika shtaka la saba, inadaiwa kati ya tarehe tofauti Januari mwaka 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshitakiwa alijipatia Sh milioni saba kutoka kwa Rose Shigela mbaye ni mtumishi wa Takukuru.
Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Agosti 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Post a Comment