Na Jacqueline Liana, Mbeya
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema iwapo viongozi na watendaji serikalini, kila mmoja atakaa sawa katika nafasi yake, na kutenda haki, changamoto zinazowakabili wananchi kwa sasa zitamalizika.
Tatizo lililopo, ni baadhi yao 'kupiga nne' tu, pasipo kuwajibika, na kuwaacha watu wakitaabika.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Daniel Chongolo, alipokuwa akihitimisha ziara ya kikazi katika wilaya za mkoa wa Mbeya, Julai 13, 2022.
Akitoa maagizo ya kutekelezwa na viongozi na watendaji wa chama na serikali katika mkoa wa Mbeya, kufuatia malalamiko ya wananchi kwamba wanakabiliwa na kero zikiwemo za ukosefu wa maji, dawa, masoko ya mazao, umeme, upungufu wa madarasa na madawati, Chongolo amesema kwamba kama kila mwenye dhamana katika chama na serikalini atatimiza wajibu, matatizo mengi ya wananchi yangepata ufumbuzi.
Katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini Mbeya, Chongolo amesema, chama hakitakuwa na simile na viongozi na watendaji serikalini na kwenye CCM, ambao hawawajibiki kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.
"Watu wanahangaika kwa kukosa huduma bora, lakini tumepiga nne tu, hatuwezi kuwa na serikali ambayo haiwajibiki kutatua kero za watu," alisema.
Aliwaambia waliohudhuria mkutano huo, wakiwemo viongozi na wataalamu wa serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, kwamba katika kuelekezana na kuhimizana kuhusu utatutizi wa kero zinazowakabili wananchi, ni lazima kuwa na uelewa wa pamoja.
"Tunakwenda taratibu kwa sasa, lakini kadri siku zinavyosonga mbele, wale wanaotukwamisha lazima tuondokane nao," alionya Mtendaji Mkuu wa CCM.
Komredi Chongolo amesema kwamba kwa viongozi na watumishi wa umma ambao wamezoea kupuuzia maagizo yanayotolewa kwa ajili ya kuwaondolea wananchi kero, waendelee na tabia hiyo.
Alisema kuna wanaodhani maagizo yanayotolewa ni porojo, lakini yeye na sekretarieti yake, wanamaanisha.
"Kama mnadhani tunafanya masihara sawa, simnajua maji hayapandi mlima, kuna siku mtajua kwamba yanaweza kupanda," alisema.
Kuanzia Julai 6 hadi 13, 2021, Katibu Mkuu Chongolo, akiwa amefuatana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM taifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, Komredi Shaka Hamdu Shaka na Komredi Kenani Kihongosi, wamefanya ziara ya kuhimizana uhai CCM mashinani, pamoja na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya.
Post a Comment