CCM Blog, Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo anatarajiwa kuwasili Visiwani hapa leo, Julai 4, 2021 kufanya ziara ya kwanza ya kikazi tangu ateuliwe na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza jana katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao alisema ziara hiyo itakuwa ya siku mbili kuanzia leo Julai 4, hadi 5, 2021.
Alisema katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Chongolo ataambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na anatarajiwa kupokelewa saa 3:00 asubuhi katika Bandari ya Malindi mjini Unguja.
Catherine alisema baadaye baada ya kuwasili, Katibu Mkuu Chongolo atakutana na Makamu Mwenyekiyi wa CCM Zanzibar, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Barazs la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema kuanzia saa 8:00 mchana Katibu huyo Mkuu na Ujumbe wake atapokelewa na wanachama wa CCM katika mzunguko wa Barabara ya Kisonge na kufanyika matembezi kuanzia hapo hadi Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Unguja.
"Atakapofika hapa katika ofisi kuu za CCM Katibu Chongolo atapokelewa kwa heshima zote za chama na kupokea gwaride la Jumuiya ya Umoja wa Vijana kisha atazuru kaburi la Rais wa kwanza hayati Abeid Amani Karume na kutumbuizwa na ngoma ya asili kabla ya kuzungumza na wanachama na wakereketwa wa chama katika viwanja vya ofisi kuu," alisema
Alisema dhamira ya ziara hiyo ni kujitambulisha na kuyasemea mambo ya Uchaguzi wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani lakini pia kupata nafasi ya kuzungumza na wazee na wafanyakazi wa Chama cha Mapinduzi(CCM).
Katibu huyo wa NEC, aliwaomba wanachama na wakereketwa kujitokeza na kumsikiliza Katibu Mkuu Chongolo juu ya muelekeo wa ilani ya CCM na utekelezaji wake kwa waliyokabidhiwa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Katibu Mkuu Chongolo anatarajiwa kuzungumza na Baraza la Wazee la Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar na wazee watano kwa kila mikoa ya Unguja ikiwemo Mjini, Magharibi, Kaskazini na Kusini.
Pia Katibu Mkuu huyo anatarajiwa kukuonana na kuzungumza na Watumishi wote wa Chama na Jumuiya zske, kwa mikoa minne ya Unguja pamoja na kupata fursa ya kuzungumza na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Catherine, alisema maandalizi ya mapokezi ya Viongozi hao katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui tayari yamekamilika.
Post a Comment