……………………………………………………………………
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Kufuatia kuwepo kwa tatizo la mawasiliano katika baadhi ya maeneo wilayani Ludewa mkoani Njombe serikali kupitia kampuni ya simu ya Airtel inatarajia kujenga minara 14 kwenye maeneo ambayo hayana mtandao kabisa huku wakazi wa kata ya Lupanga wakibahatika kupata minara miwili.
Hayo ameyasema mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara katika kata ya Lupanga kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi ambapo wananchi wa kata hiyo walihoji juu ya kupata mawasiliano ya uhakika kwakuwa kwa sasa maeneo hayo hakuna mtandao wa simu yeyote unaoshika.
Mbunge huyo amesema kuwa minara hiyo itasambazwa katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya mtandao hasa maeneo ya mwambao ambako watu wa maeneo hayo hawana maeasiliano kabisa.
Aliongeza kuwa wakazi wa mwambao wanajihusisha zaidi na shuguli za uvuvi hivyo endapo minara hiyo itakamilika itawasaidia kufanya mawasiliano kwa urahisi na wateja wao waliopo maeneo ya mijini.
“Kwa karne ya sasa mawasiliano ni kitu muhimu sana kwa jamii kwani sasa hivi watu hufanya biashara, kutafuta kazi na mengineyo kupitia simu hivyo kutokana na umuhimu wake serikali imeamua kututatulia tatizo hili la mitandao”, alisema Kamonga.
Aidha kwa upande wa wananchi hao wameishukuru serikali kwa hatua hiyo kwani wamekuwa wakipata tabu ya mawasiliano kwa kipindi kirefu.
Godfrey Nziku ni mmoja wa wananchi hao ambaye pia alipata bahati ya kuwasiliana na meneja wa kampuni ya Airtel juu ya mahali wanapoweza kufunga minara hiyo.
“Niliwasiliana na meneja kampuni ya simu ya Airtel ili niwaelekeze mahali pakufunga minara na nilifanya hivyo na baada ya hapo waliniambia tutaendelea kuwasiliana”, Alisema Nziku.
Naye Anastancia Mtega ambaye pia ni mwananchi wa eneo hilo amesema hatua hiyo iliyofikiwa ni neema kubwa kwao hivyo kuna kila sababu ya kuishukuru serikali pamoja na mbunge wao kwa kufikisha kilio chao.
Ameongeza kuwa kwa sasa hawapati mtandao kabisa hivyo wanapotaka kufanya mawasiliano wanalazimika kwenda maeneo ya kata za jirani yanayoshika mtandao ili kukamilisha mawasiliano hayo.
Pia alimpongeza mbunge huyo kwa kuendelea kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao kwani awali alipowasili katika kata hiyo walimueleza ugumu wa mawasiliano walionao ambapo utekelezaji wake tayari umeanza na sasa kurejea tena kusikiza changamoto nyingine walizonazo.
Ziara hiyo ya mbunge wa Ludewa bado inaendelea na mpaka sasa tayari ametembelea vijiji 22 ambavyo ni Lihagule, Kingole, Kiyogo,Liughai, Lifua, Luilo, Kipangala, Idusi, Nkomang’ombe, Iwela, Muhumbi, Kimelembe, Ligumbilo, Lufumbu, Mlangali, Itundu, Utilili, Lusala, Lupanga, Masimbwe, Kiyombo na Mkiu.
Post a Comment