Ikulu, Dar es Salaam, leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, Jaffar Haniu, leo, imesema Blair ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) amemhakikishia Rais Samia kuwa taasisi yake inaunga mkono jitahada mbalimbali anazochukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Amesema taasisi yake inafanya kazi katika nchi 16 Afrika ikijikita kutekeleza vipaumbele vya Serikali zao ambapo amsema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu taasisi yake imejikita zaidi katika masuala ya kukabiliana na janga la UVIKO 19.
Blair amesema katika kukabiliana na janga la UVIKO 19, taasisi yake inashughulika zaidi na masuala ya upimaji na usambazaji wa chanjo ambapo amesema taasisi yake inaweza kusaidia Tanzania kuwafikia wazalishaji wa chanjo hizo.
Aidha, amesema mbali na masuala ya UVIKO 19, pia wanajengea uwezo nchi washirika kufuatilia miradi ya kilimo, nishati na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Blair kwa kumjulisha masuala yanayofanywa na taasisi yake katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nchi washirika.
Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.
Kuhusu UVIKO 19, Rais Samia amemueleza Blair kuwa tayari Serikali ina mpango wake wa Kitaifa kuhusu namna ya kushughulikia masuala yote ya UVIKO 19 ikiwemo uratibu wa chanjo.
Rais Samia amesema katika kujijengea uwezo kwa sasa Serikali ina mpango wa kujenga viwanda vya kuzalisha chanjo za aina mbalimbali na hivyo kuomba taasisi ya Tony Blair kuunga mkono jitihada hizo.
Aidha, Rais Samia ameikaribisha taasisi ya Tony Blair kuja nchini kufanya kazi na taasisi za Tanzania kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair wakati Blair alipofika Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 22,2021. (Picha na Ikulu)
Post a Comment