Featured

    Featured Posts

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MAONESHO YA KIKANDA YA UTALII YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI MWEZI OKTOBA 2021

 


 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza kwenye  Mkutano wa Kisekta wa  Baraza la Mawaziri  wa Utalii na Wanyamapori wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya Mtandao jana  akiwa Jijini Arusha ambapo amewaeleza Mawaziri hao kuwa Tanzania ipo tayari kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda wa Utalii wenye lengo la kutangaza kwa pamoja fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo, mkutano huo utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu Jijini Arusha
………………………………………………………………..
Tanzania inatarajia kuwa Mwenyeji wa Maonesho  ya   Kikanda ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC Regional Tourism EXPO)  yatakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu Jijini Arusha.
Akizungumza  jana  Jijini Arusha kwenye Mkutano wa Kisekta wa  Baraza la Mawaziri  wa Utalii na Wanyamapori wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya Mtandao,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro aliwaeleza  Mawaziri hao kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa Maonesho hayo huo.
Waziri Ndumbaro alilitoa ombi hilo mara baada ya Burundi aliyetakiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho hayo kutokuwa tayari kuyafanya kwa  mwaka huu na hivyo  kuahidi kuwa atakuwa tayari mwakani,  hali hiyo ikailazimu Tanzania kuomba na kisha  kukubaliwa kuwa Mwenyeji wa Maonesho hayo.
Alisema lengo la Maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo  ni kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi hizo. 
Alisema makubaliano hayo ya kuanzisha maonesho hayo ni hatua mahsusi kwa  nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kujitangaza baadala ya kutegemea makampuni makubwa ya utalii kutoka nje  kutangaza vivutio vilivyopo katika Jumuiya  hiyo kwa namna yanavyotaka yenyewe.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amewaelezea Mawaziri hao kuwa maonesho hayo ya  Utalii  nchini Tanzania kufanyika kwake itakuwa ni hatua muhimu ya  kuwatia nguvu sekta binafsi ya kuona namna ya kujipanga upya kurudi  katika biashara ya utalii kutokana na ugonjwa wa UVIKO kuitikisa vibaya sekta hiyo.
Alisema athari za ugonjwa wa UVIKO 19 umedumaza Makampuni binafsi yanayojihusisha na utalii na hivyo kupelekea  kupunguza idadi ya wafanyakazi wa sekta na hivyo kuongeza tatizo kubwa la ajira nchini
” Kwa vile Burundi imeonesha kutokuwa tayari, Sisi Tanzania tupo tayari kufanya Maonesho hayo kwa mwaka huu ikiwa lengo letu kutuma ujumbe kwa mataifa makubwa kuwa tupo tayari kuwapokea na kuwahudumia watalii” alisisitiza Dkt.Ndumbaro
Katika hatua nyingine Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuomba muda zaidi wa  kujiandaa kujiunga kwenye Visa ya pamoja  ya Utalii.
Akifafanua katika mkutano huo, Waziri Dkt.Ndumbaro aliwaeleza Wajumbe hao kuwa suala viza ya pamoja ya utalii kwa Tanzania ni suala nyeti na  linahusisha mamlaka zaidi ya moja katika kufanya maamuzi hivyo inaomba ipewe muda zaidi kwa ajili ya kuweza kufikia maafikiano na mamlaka zingine hususana mamlaka ya uhamiaji na usalama.
Alisema  suala la visa ya pamoja ya utalii linahitaji makubaliano ya ndani kwanza kabla Tanzania haijaamua kujiunga nayo suala  ambalo mjadala wake wa kuitaka Tanzani kujiunga liliungwa mkono kwa nguvu sana na Mawaziri wa kutoka nchini   Kenya pamoja  na Uganda 
Licha ya mjadala huo kuchagizwa na Mawaziri hao, Dkt.Ndumbaro alisema suala la viza ya pamoja ni muhimu kibiashara lakini linagusa usalama wa nchi na hivyo aliwashauri Mawaziri hao liache liamuriwe na mamlaka zingine ikizingatiwa kuna Tanzania bara na Tanzania Visiwani.
Katika Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wote wenye dhamana ya utalii na wanyampori  kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzania, Kenya Uganda, Sudani pamoja na Rwanda. 
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana