Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akipata maelezo juu ya maendeleo ya ujenzi wa hosteli ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kutoka kwa Mkuu wa Chuo Richard Mganga alipotembelea eneo hilo Julai 17, 2021. Nyuma ni Mkururugenzi Msaidizi wa Michezo Addo Komba, kulia Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Johari Samizi
Mafundi wakiendelea kufyatua matofali kwa ajili ya kujengea hosteli ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya itakayokuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanachuo 190.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akihutubia kwenye mahafali ya kumi (10) ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Julai 17, 2021.
Wanachuo wa chuo cha Michezo Malya waonyesha mchezo wa kufanya mazoezi kwenye mahafali ya kumi (10) ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Julai 17, 2021.
********************
Na John Mapepele, Mwanza.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ameutaka Uongozi wa Chuo cha Michezo Malya kukamilisha kazi zote za ujenzi wa hosteli ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanachuo 190 ifikapo Septemba mwaka huu ili lengo la Serikali la kufanya upanuzi wa chuo hicho kuwa miongoni mwa kituo kikubwa cha michezo barani Afrika liweze kufikiwa.
Mhe. Gekul ameyasema hayo Julai 17, 2021 alipotembelea eneo la ujenzi wa hosteli hiyo kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu 107 kwenye mahafali ya kumi (10) ya Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Mhe. Gekul amesema hadi sasa tayari Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 300 kwa ajili gharama za awali za hosteli hiyo, na shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu mbalimbali ya kukifanya chuo hicho kuwa kituo cha michezo cha kimataifa.
Ninapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia kwa kutoa kipaombele kwenye Sekta ya Michezo na kutupatia fedha nyingi ili ziweze kukifanya chuo hiki cha Malya kuwa miongoni mwa vyuo vikubwa barani Afrika na duniani. Amesisitiza Mhe. Gekul.
Amezitaka Halmashauri na Wilaya zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya michezo ili zoezi la kuhamasisha michezo kuanzia ngazi ya kijiji liweze kufanikiwa na hatimaye kuimarisha afya na kupunguza baadhi ya magonjwa.
Amesema Chuo cha Malya ni kitovu cha kuibua wataalam wa michezo ambapo amefafanua kuwa baada ya upanuzi huu taifa litanufaidika kwa kupata wachezaji na wataalam wa michezo ambao watakuwa na kiwango cha kimataifa.
Amezitaka halmashauri na wadau mbalimbali kuleta wanafunzi kwenye chuo hiki ili waweze kunolewa katika taaluma za michezo zinazotolewa chuoni hapo kwa kiwango cha kimataifa.
Amepongeza halmashauri na mikoa iliyowaleta walimu na watumishi mbalimbali kuja kusomea kozi mbalimbali za michezo ili kuinua michezo ambapo ametoa rai kwa halmashauri ambazo bado hazijaleta watumishi katika chuo hiki kuwaleta ili halimashauri zao ziwe na wakufunzi wenye taaluma.
Akitoa taarifa kwa Mhe. Gekul, Mkuu wa chuo hicho, Richard Mganga amesema katika mahafali haya wanachuo 107 wamehitimu kozi za Stashahada ya Elimu katika Michezo (Ordinary Diploma in Physical Education and Sports) wanachuo 41, Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji Michezo (Ordinary Diploma in Sport Coaching Education) wanachuo 23, na Diploma ya Uongozi na Utawala katika Michezo (Ordinary Diploma in Sports Management and Administration) wanachuo 43.
Mganga amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 chuo kilitoa mafunzo kwa wadau wapatao 1,445 ambapo kimevuka lengo lake la kutoa mafunzo kwa wastani wa wadau 300 kila mwaka katika vituo vyake vya Dar es salaam, Malya na Tunduru.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Johari Samizi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya maboresho ya Chuo cha Michezo cha Malya ambapo pia amewataka wananchi wa Wilaya yake kuendelea kuchua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19.
Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo Addo Komba amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata vizuri ambapo amesisitiza kuwa vyeti walivyovipata vitapimwa kwa kazi watakazokuwa wanazifanya.
Pia amewataka kwenda kufufua na kuboresha michezo na klabu za riadha ambazo amesema zilianzishwa na Mhe. Rais wakati alipokuwa Makamu wa Rais.
Kwa kwenda kuendeleza jogging klabu mtakuwa mnaunga mkono jitihada za Mhe. Rais kwa kuwa tayari alishafanya kazi kubwa ya kuzianzisha nchi nzima nzima kilichobaki ni kuendeleza tu alifafanua Mkurugenzi Komba.
Post a Comment