Na Mwandishi wetu
SERIKALI imeonya Watoa Huduma wanaojihusisha na udanganyifu katika uchakataji wa madai ya huduma za matibabu wanayoyawasilisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kuwataka waache mara moja.
Aidha kwa baadhi ya watoa huduma ambao tayari walishawalisha madai kwa Mfuko yenye udanganyifu na badae yakagundulika wajiandae kurejesha fedha kwa kuwa Serikali haiwezi kukubaliana na vitendo hivyo vyenye kulenga kudhoofisha huduma za afya.
Onyo hilo lilitolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF pamoja na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF tangu kuanzishwa kwake.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa NHIF kwa kukata utepe wa nyaraka za kazi za kumkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Bw. Juma Muhimbi (kushoto).
“Wote waliofanya udanganyifu katika madai ya Mfuko huu au kutumia taaluma zao kwa ubadhilifu naomba niwape taarifa mapema kwamba wajipange kuzirejesha fedha hizo na kwa wale ambao bado wanaendelea na vitendo hivi ni bora waache mara moja kwa kuwa tukibaini hatua kali dhidi yao zitachuliwa na katika hili niseme wazi kabisa kuwa nitalishughulikia mwenyewe ninachohitaji ni ushahidi tu na Mkurugenzi Mkuu nataka kila robo mwaka unipatie taarifa ya malipo yanayofanywa ili tuweze kujenga huu uaminifu ,” alisema Mhe. Dkt. Gwajima.
Ili kuweza kupambana na hali hiyo aliiagiza Bodi ya Mfuko kuhakikisha inasimamia na kuitangaza Sera ya Mfuko ya utoaji wa taarifa kwa siri (Whistle Blower Policy) ili wananchi wajue wanatoaje taarifa hizo ambazo zinalenga kukomesha udanganyifu wa kihuduma za matibabu
. Sehemu ya Watumishi wa NHIF wakifuatilia tukio la uzinduzi wa Bodi ya NHIF na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma katika Vituo vya kutolea huduma, alisema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana lakini pia akatumia nafasi hiyo kuwataka watoa huduma kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo inayotolewa na Mfuko.
“Hii fursa ipo hakikisheni watoa huduma mnaitumia badala ya kukaa mlalamika kukosa baadhi ya mahitaji, Mikopo hii ipo na inatolewa na masharti nafuu sana hivyo sitarajii kusikia mtoa huduma analalamika hana bajeti ya kununua vifaa,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima alizungumzia utekelezaji wa suala la Bima ya Afya kwa Wote ambapo aliuhakikishia umma kuwa Muswada wa sheria unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni mwezi Septemba na kwa upande wa Wizara yake tayari maandalizi yote yameshakamilika.
Picha ya pamoja na Bodi mpya ya NHIF iliyozinduliwa na Mhe. Waziri Gwajima.
Alitoa maagizo kwa Bodi mpya ya NHIF kuhakikisha inasimamia uendelevu na uimarishaji wa Mfuko pamoja na kuhakikisha wananchi walioko katika maeneo ya vijijini wanafikiwa na huduma hizo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Bwana Juma Muhimbi, alisema kuwa yeye na bodi yake watahakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia matarajio makubwa ya Serikali na wananchi waliyonayo katika Mfuko huo.
“Tunafahamu tuna kazi kubwa mbele yetu, Mfuko huu umebeba matumaini ya wananchi hivyo Bodi itasimamia ili yote yanayotarajiwa yaweze kufanyika na wananchi wapate huduma kupitia mfumo wa Bima ya Afya na kuhakikisha tunazingatia yote uliyotuelekeza leo,” alisema Bw. Muhimbi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Benard Konga akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa lengo la Mfuko ni kuhakikisha unasogeza huduma zake kwa wananchi ili wasipate changamoto yoyote katika kupata huduma za bima ya afya.
“Mfuko umezidi kuboresha huduma zake kwa wanachama na watoa huduma na kwa sasa tumeanza kufanya kazi na watoa huduma kwa njia ya mtandao wa kielectroniki ili kurahisisha uwasilishaji, uchakataji na ulipaji wa madai na kuondokana na malalamiko ambayo yanaweza kuzuilika. Mpaka sasa jumla ya watoa huduma 40 wamejiunga na mfumo huu na tumejipanga utaratibu huu utumike na vituo vyote kwa kuanzia na ngazi ya Hospitali za ngazi ya mkoa hadi taifa,” alisema Bw. Konga.
Mhe. Waziri Dkt. Gwajima akizindua rasmi kuanza kwa maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF kwa kukata utepe wa nembo ya maadhimisho hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi aliyemaliza muda wake Spika Mstaafu Mhe. Mama Anne Makinda alishukuri Mfuko na Wizara kwa kushirikiana na bodi aliyoiongoza iliyomaliza muda wake kwa kazi kubwa iliyofanywa na bodi yake ikiwemo uanzishwaji wa Vifurushi vya Bima ya Afya ambavyo vinamwezesha kila mwanachi sasa kujiunga na kunufaika na huduma za bima ya afya.
Post a Comment