WAZIRI wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza Familia ya Liginiku Millinga na mkewe Upendo Ngoda kwa kujitoa na kuanzisha kituo cha kulea watoto watokao katika mazingira magumu kijulikanacho kama Jerusalem Home of Orphanage na kutoa huduma muhimu za afya, lishe bora, malazi na elimu na kuwataka wadau wa maendeleo na wafadhili kuunga mkono jitihada hizo ili kituo hicho kiweze kufikia malengo ya kupanua huduma ya kulea watoto yatima 100 ifikapo 2024.
Amesema kuwa kituo cha Jerusalem kimekuwa kikizingatia haki za watoto hao na kutoa malezi bora kwa ujenzi wa taifa imara la baadaye na kuwataka watanzania na wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo ili kukiwezesha kituo hicho kulea watoto wengi zaidi katika mazingira salama zaidi.
Kwa upande wake mwanzilishi na Mama mlezi wa kituo hicho Upendo Ngoda amesema, kituo hicho kinalea watoto 16 wenye umri wa kuanzia siku moja hadi miaka 6 na wamekuwa wakipambana na changamoto zilizopo na kuwajibika katika kuhakikisha wanawajenga watoto hao katika misingi imara.
Bi. Upendo amesema, jamii na marafiki wa Jerusalem wamekuwa sehemu kubwa ya kushiriki katika kuhakikisha watoto hao wanapata huduma zote muhimu ikiwemo afya bora, bima za afya pamoja na elimu bora.
Vilevile amesema katika huduma hiyo ya malezi hadi sasa wamefanikiwa kuwaunganisha watoto wanne na familia zao.
Kuhusiana na changamoto zinazokikabili kituo hicho bi. Upendo amesema hakuna chanzo cha kudumu cha mapato wala wafadhili bali kituo hicho kinalelewa na jamii na marafiki pamoja na ufinyu wa eneo la kutolea huduma hiyo hali inayopelekea kushindwa kuwachukuwa watoto wengi zaidi kwa kuwa uwezo wa kituo ni kubeba watoto 18 pekee.
Post a Comment