Na Pius Ntiga, Dar es Salaam.
Makumbusho ya Taifa Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya A Plus Communications, wameandaa Maonesho ya Vitabu Tanzania yatakayoshirikisha Waandishi wa Vitabu kutoka ndani na nje ya nchi ili kujenga chachu ya wananchi kupenda kusoma Vitabu.
Lengo ni kuwakutanisha pia Waandishi wa Vitabu, Wasomaji wa Vitabu, Wachapishaji, Wauzaji na Maktaba kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo wataonesha kazi zao za Uandishi na kuuza Vitabu vyao.
Mkurugenzi wa Kampuni ya A Plus Communications, Humphrey Millinga, amesema tahadhari zote zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona (Uviko-19) wakati wa maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika kwenye Viwanja vya Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 hadi 28 August 2021, zinachukuliwa.
Aidha, kabla ya maonesho hayo Jumatano wiki hii ya Agosti 11 mwaka huu, wadau wa Vitabu na Waandishi wa Vitabu zaidi ya 40 wanatarajia kukutana katika Makumbusho ya Taifa katika mjadala wa masuala ya Vitabu, ambapo pamoja na mambo mengine watajadili na kujiuliza ni kwa nini wananchi wengi hawapendi kusoma Vitabu.
Milinga amesema maonesho hayo yanatarajiwa kuvutia idadi kubwa ya wadau ikiwemo, Wasomi, Wanazuoni, Wanafunzi, Walimu, wapenzi Wasomaji wa Vitabu na Majarida ambapo watapata nafasi ya kupata Vitabu na machapisho tofauti katika Fasihi, Hisitoria, Mashairi, Maigizo, Riwaya, Tamthilia, hadithi za kubuni na za kweli.
Maonesho hayo yanatajwa kuwa yameandaliwa ili kulenga kuamsha uelewa miongoni mwa watu kuhusu umuhimu wa kusoma Vitabu, jisni ya kuchagua vitabu vizuri kwa ajili ya watoto, wanafunzi na kwa ajili ya matumizi binafsi.
Aidha, tukio hilo litatoa maarifa kwa watu kuhusu namna ya kutunza Vitabu na jinsi ya kujipatia mbinu mbalimbali za kusoma Vitabu.
Pia katika tukio hilo waandishi wa Vitabu na wadau wengine wa Vitabu watapata fursa ya kuchangia vitabu kwa Makumbusho ya Taifa, ambapo Vitabu hivyo vitatunzwa kwenye Maktaba ya Makumbusho kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.
Milinga amesema Makumbusho ya taifa inatoa fursa hiyo kwa waandishi wa vitabu pamoja na wadau wengine wa vitabu ili kuzifanya kazi zao za fasihi ziweze kutunzwa katika sehemu salama na inayoheshimika zaidi katika nchi, itakua heshima kubwa kwa waandishi wa Vitabu pamoja na wadau wengine wa vitabu kuzifanya kazi zao za fasihi zikatunzwa kwenye makumbusho ya taifa.
“Utafiti wa kina haukufanyika kubaini tabia ya usomaji wa Vitabu kwa Watanzania, lakini hata kwa mtazamo wa kawaida inajidhihirisha kwamba kipaumbele cha usomaji wa vitabu kipo chini sana na kwamba hii inazolotesha na kudhoofisha ustaarabu” alisema Milinga.
“Wadau wa Vitabu wanakiri upungufu wa watu wenye kupenda kusoma Vitabu ikiwemo watoto na vijana, hasa usomaji wa vitabu vya ziada ambavyo havihusiani na vitabu ya kiada” Alisema Milinga.
Aidha, Milinga amesema Wanafunzi wengi wanapoteza muda katika kubadirishana jumbe za simu, badala ya kuwekeza katika usomaji wa vitabu vilivyo ndani na nje ya mtaala, hivyo uwepo wa maonesho hayo itasaidia kuamcha ari ya usomaji wa Vitabu.
Maonesho hayo ya Vitabu Tanzania yanatajwa kuwa yataamsha ari ya usomaji wa Vitabu kwa Watanzania, kuleta uelewa kuhusu umuhimu wa usomaji wa vitabu na faida zake, na kuhamasisha usomaji wa vitabu miongoni mwa Watanzania.
Pia Milinga amesema maonesho hayo yataongeza uhitaji mkubwa wa vitabu Tanzania, Kutengeneza mwanya kwa wapenzi wa vitabu kujipatia Vitabu wanavyovitafuta kwa shauku, Kutengeneza na kuimarisha mtandao na mshikamano miongoni mwa Wasomaji na wapenzi wa Vitabu, Waandishi na Wachapishaji wa Vitabu.
Kauli mbiu ya maonesho hayo ya Vitabu Tanzania ya mwaka 2021 ni “Soma Vitabu; ongeza Maarifa”.
Post a Comment