Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh. Bilioni 300 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Makao Makuu ya nchi Dodoma, kufuatia dhamira yake ya kuendeleza miradi yote ikiwemo ya ujenzi wa Makao Makuu na miradi mbalimbali inayofanyika Dodoma.
Hayo yametamkwa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Ikulu mpya Chamwino, Dodoma ambao umefikia asilimia 78.
“Ujenzi wa Makao Makuu bado unaendelea, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kazi zote ziendelee zikiwemo za ujenzi wa mji wa Serikali hapa Dodoma.” akasema Waziri Mkuu.
Amesema, kati ya fedha hizo, Sh. Bilioni 131 zitatumika katika ujenzi wa majengo ya maghorofa ya makao makuu ya wizara kwenye Mji wa Serikali, Mtumba na Sh. Bilioni 169 zitapelekwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya maboresho ya jiji hilo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na umeme.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama akutane na Mawaziri wenzake ili waanze mchakato wa ujenzi majengo ya wizara akisema ujenzi huo unatakiwa uanze mwezi ujao na ufanywe na Kampuni za Ukandarasi za Serikali pamoja na Kampuni za Sekta binafsi.
Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo na hatua iliyofikiwa na kwamba ana imani utakamilika kwa wakati.
“Leo nimefarijika kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huu na furaha hii inatokana na hatua tuliyoanzia na tulipofikia sasa. Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitaka kuona Ikulu mpya inafanana na ya Dar es Salaam na leo nimeona kweli zinafanana.” amesema Waziri Mkuu.
Post a Comment