***************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WABUNGE wa Mkoa wa Manyara, wameipongeza kwaya ya Ingera-Emoipo (watoto wa Moipo) ya Kata ya Ruvu Remit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa namna inavyotumbuiza nak ufikisha ujumbe kupitia nyimbo zake.
Kwaya hiyo imeimba wimbo maalum wa kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametembelea mji mdogo wa Mirerani leo Septemba 5 ili kurekodi filamu ya utalii kwenye madini ya Tanzanite.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Wakili msomi Edward Ole Lekaita amesema kwaya ya Ingera-Emoipo, imekuwa inafanya kazi za viongozi wa kuchaguliwa kwa kueleza kero za jamii serikalini.
Mbunge wa Jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amesema kwaya hiyo imeeleza kero za jamii hivyo kumsaidia mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka.
“Mnafanya vyema kwa kuimba changamoto za maji, elimu na afya kwa kweli mnasaidiana na mbunge wenu Ole Sendeka katika kufikisha kilio chenu,” amesema mhandisi Hhayuma.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Philip Gekul ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini aliwapongeza wanakwaya hao kwa kuonyesha kipaji chao na kutoa ujumbe mzuri kupitia wimbo wao.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu mjini, Paul Zacharia Isaay amesema kwaya hiyo inapaswa kuimba mambo ya mkoa mzima wa Manyara kama ilivyofanya kwa kuelezea changamoto za Simanjiro.
“Mnaimba mambo mazuri kwa kweli ila inabidi sasa muwe mnaimba changamoto za mkoa mzima na siyo wilaya ya Simanjiro peke yake,” amesema Isaay.
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo amewapongeza wana kwaya hao kwa namna wanavyofikisha ujumbe wao kwa hadhira inayowazunguka.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay amesema kwaya hiyo inapaswa kuungwa mkono kwani imeonyesha ujumbe kwa kutaja changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo maji kupitia sanaa.
Mbunge wa vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga amesema wanakwaya hao ni wakuungwa mkono ili waendelee kuonyesha uwezo wao wa kufikisha ujumbe kwa njia ya nyimbo.
Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege amewapongeza wanakwaya hao wa Ingera-Emoipo kwa namna walivyofikisha ujumbe kwenye ziara hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amewashukuru wabunge hao kwa namna walivyoipongeza kwaya hiyo ya kutoka kijiji cha Lerumo kata ya Ruvu Remit.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Mosses Komba amesema kwaya hiyo ina waimbaji 180 ila walifika wanakwaya 30 ili kutumbuiza kwenye ziara hiyo ya Rais Samia.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema kwaya ya Ingera-Emoipo ni mahiri kwa uimbaji kwani hivi karibuni kwaya hiyo ilifanya harambee na kupatikana shilingi milioni 125.
Post a Comment