Viongozi wakiwa katika mafunzo kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi ambapo kambi hiyo maalumu ya mafunzo kwa viongozi wapya wa TGGA, ikiendelea. Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo yameanza Septemba 12, yatamalizika Ijumaa Septemba 17, 2021.
Viongozi wakiendelea na mafunzo kwa njia ya vikundi kwenye viwanja vya shule hiyo leo.
Mdau, nakuomba uendelee kusikiliza kupitia clip hii ya video, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TGGA, Maembe akitoa mafunzo hayo lakini pia baadhi ya viongozi wapya wa TGGA wakielezea jinsi walivyoyapokea na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi....
Clip hii ya Video imeandaliwa na Richard Mwaikenda
Mhariri Blog ya Taifa ya CCM
0754264203
Mada hii ya Uongozi ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TGGA, Anna Maembe katika mafunzo kwa viongozi wa TGGA,
Moshi, Tanzania 12/9/2020- 17/9/2021.Mpangilio wa mada:
Maana ya uongozi.
Aina za uongozi.
Kiongozi bora ni yupi?.
Maadili na Miiko ya uongozi.
Hitimisho.
Rejea
Uongozi ni nini?
Uongozi ni mamlaka au karama ya kuwaonesha watu njia kwa vitendo ili kufika malengo tarajiwa. Uongozi ni kushirikiana na waongozwa na kuweka maono (au Dira) ambayo itawezesha kufika malengo/ maendeleo tarajiwa.
Kiongozi lazima awe muadilifu na mnyenyekevu, kiongozi ni mtu awezaye kuongoza njia ili kufikia jambo tarajiwa, pia awe na uwezo wa kushawishi na kuwavuta wengine ili wamfuate na “kutembea” pamoja kimatendo kufikia lengo tarajiwa.
Kiongozi lazima awe na uwezo wa kuwashawishi na kuwaunganisha watu, na kuwawezesha kutumia karama, vipawa na talanta au rasilimali walizonazo kwa ajili ya kujiletea maendeleo tarajiwa.
Katika kila kundi la vitu (wadudu, wanyama au watu) lazima kuwe na kiongozi Bila kuwa na kiongozi, hakutakuwa na muelekeo wa pamoja.
Aina za uongozi.
Kuna aina kadhaa za uongozi, kwa leo nitaelezea aina tano tu za uongozi:
Uongozi wa malengo (management by objectives)
Aina hii ya uongozi huhitaji na kutumia majadiliano ambapo washiriki hutoa mawazo yao ambayo hujadiliwa na kufikia muafaka, Uongozi huu pia hufikiwa kwa njia ya demokrasia na muafaka.
Uongozi wa kuzunguka (rotational).
Huu ni uongozi ambao kiongozi huwazungukia waongozwa katika maeneo yao na kukusanya taarifa na kukagua na siyo kusubiri kuletewa taarifa au kuamini taarifa unayopewa (trust no- body).
Uongozi wa kiana (Exceptional)
Kiongozi hugawa madaraka kwa kuangalia anaefanya kazi kwa kujituma kuliko wengine. Aidha huweza kummotisha anaejituma zaidi.
Uongozi wa mabavu (intimidation/ autocracy)
Unahitaji utekelezaji wa haraka bila kuhoji.
Uongozi wa kutojali (lazier faire)
Ni uongozi wa kuruhusu mtu kufanya kazi anavyotaka bila kubanwa na mtu yeyote.
Hizi zote ni aina muhimu za uongozi na mara nyingi kiongozi unapaswa kutumia zaidi ya aina moja ya uongozi ili kufikia malengo tarajiwa.
Kiongozi bora ni Yupi?
Kiongozi ni mtu anaeongoza na kuwa kioo cha watu. Anawaongoza watu na kuwaonesha wapi panapofaa kwenda. Anawaongoza katika njia sahihi ili wasipate madhara.
Kwa hiyo kiongozi lazima awe mwadilifu, mnyenyekevu, msikivu na mwenye maono/ DIRA (iliyofikiwa kwa kushirikisha waongozwa/wadau). Lazima awe muwasilishaji mzuri (good communicator).
DIRA lazima iwe na malengo ya kwenda mbali (20-100 years), kwa hiyo kiongozi bora ana wajibu wa:-
Kuwaongoza wenzake na kuwafikisha salama sehemu lengwa.
Kuwafundisha na kuwaelekeza yanayofaa kutenda kwa kuwaelekeza (mara nyingi kwa vitendo).
Kiongozi ni kioo cha kuigwa na anaowaongoza.
Kiongozi lazima awe mfuatiliaji na kutoa mrejesho/ masahihisho na pongezi.
Kiongozi anatengenezwa/ analelewa kwa muda mrefu kabla hajawa kiongozi bora.
(John Ulanga (2019); Nguzo kuu za uongozi Bora 360 Clouds media).
Kiongozi bora lazima ayaishi maadili ya uongozi.
Kusoma na kutengeneza wataalamu bali viongozi wanalelewa (murtured)
Kiongozi lazima awe na akili, nguvu na uadilifu na (intellectual curiosity na Emotional intelligency (EI) ei, akili ya maisha cf. IQ.
Kiongozi lazima awe mtu wa kutoa “MATUMAINI”, wanaoongozwa waamini kuwa tunakokwenda hali ni nzuri zaidi kuliko sasa.
Kiongozi lazima ajifunze kujiongoza yeye mwenyewe kwanza (maisha yako, familia, mtaani, kundi dogo, makundi etc.) ili na wengine waweze kukuamini kuwa unaweza kuwaongeza. Nani anataka kungozwa na mlevi, mgomvi, mwizi, mkabila, mchoyo etc?.
Kiongozi lazima asikilize maoni ya watu na akubali kukosolewa na we tayari kujifunza mambo mapya na kutoka kwa wengine.
Kiongozi lazima awe na nidhamu katika utendaji wake.
Kiongozi bora ni Yule anayegawa majukumu (to delegate).
Kiongozi bora ni Yule anayeandaa viongozi wengine watakaomrithi atakapotoka madarakani.
Maadili na miiko ya uongozi.
Maadili ni mwenendo au tabia njema inayokubalika na jamii katika uongozi ili kufikia malengo na kujiletea maeneleo.
Kiongozi lazima awe na maadili katika utendaji kazi wake awe na heshima na atoe haki kwa wote, usawa na awe na matumizi bora ya rasilimali.
Kiongozi hapaswi kuangalia maslahi yake binafsi, lazima aone na kutanguliza maslahi ya kikundi au taasisi anayoiongoza.
Kiongozi aoneshe uongozi kwa vitendo.
Kiongozi asiwe mla rushwa, mbaguzi, mlevi n.k.
Kiongozi awe msikivu wa maoni ya wote.
Kiongozi ahakikishe makundi yote yana shiriki katika kufikia malengo (no one should be left behind).
Aheshimu muda wa kazi na kuhakikisha anawapa watu nafasi ya kupumzika.
Aheshimu maoni ya wataalamu na kuwasikiliza.
Atekeleze na kusimamia sheria, kanuni, Taratibu na mingozo ya sehemu ya kazi na ya nchi.
Afuatilie na kuhakikisha kazi zote zinatekelezwa kwa uadilifu na taarifa zinaandaliwa na kufikishwa sehemu husika.
Ahakikishe Rasilimali zote ( Fedha, mali na Watu) zinatunzwa.
Aruhusu watumishi kujiendeleza kitaaluma na kushiriki katika vyama vya kitaaluma.
Aweze kujizuia kuonesha hisia kali (binafsi, kisiasa, kidini nk.) zinazoweza kusababisha mgawanyiko na uvunjifu wa amani sehemu za kazi.
Hitimisho.
Uongozi ni mada pana inayoweza kuelezewa kwa mawanda mapana. Aidha uongozi unaanza pale wanapokuwepo viumbe (wadudu,wanyama na binadamu) zaidi ya mmoja ili kuweza kuwa na mpangilio matendo yao. Hata sisimizi wanaenda kwa kuongozwa, watoto wanapocheza lazima mmoja wao anawaongoza wengine. Ili kuwa kiongozi bora ni lazima sheria, kanuni, taratibu, miongozo ifuatwe.
Viongozi lazima wafuate maadili na miiko ya uongozi, kuweka na kusimamia dira ya Taasisi na kutumia rasilimali kwa uadilifu mafanikio kwa pamoja. Viongozi lazima waheshimu watu wote na kutenda haki kwa wote.
Aidha kila upatapo uongozi katika ngazi yoyote ile ni wajibu wako kujielimisha na kuelewa miiko na maadili yakupasayo kufuata ili kuweza kufikia matarajio na malengo ya kazi uliyoaminiwa kutekeleza.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.
6.0 Rejea
Nyerere, J. K (1967)
Azimio la Arusha
Ulanga, J (2020)
Sifa za kiongozi Bora.
Joel Nanauka (2019)
Mambo matano ya kufanya uwe kiongozi mzuri.
Nyerere J.K (1995)
Kiongozi Bora ni Yupi
IPP Media (2018)
Sifa kumi za kiongozi mzuri ndani ya Taasisi.
http://knowpolitics.org (2003)
Uongozi Bora: Kitabu cha mafunzo ya uongozi kwa wanawake.
Post a Comment