Kanisa Halisi la Mungu Baba lenya Makao yake Makuu Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam, limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kufanya kazi zake bila kuwa na hofu yoyote kwa kuwa wapo Watanzania wengi wanaompenda na kumuunga mkono na kama wapo wanaomchukia basi ni wachache sana.
Hayo yamesemwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, Baba Halisi, akimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani, Masauni Hamad Masauni wakati wa Ibada ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu, iliyofanyika jana katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, ambapo Masauni alikuwa mgeni rasmi.
"Mheshimiwa Waziri, kuna watu waliposikia nakuja kufanya Ibada hii ya kuliombea Taifa amani na utulivu, waliuliza, kuna jambo nimesikia? Kwa kweli hakuna chochote kibaya nilichosikia, isipokuwa tunafanya ibada kama hii kwa kuwa ni majira yake.
Tunakuomba utufikishie salam zetu kwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, mwambie tunampenda sana, na siyo sisi tu tunaompenda na kumuombea mema, wapo Watanzania wengi wanaompenda na kama wapo wanaomchukia basi ni wachache sana.
Mwambie afanye kazi zake bila hofu wala wasiwasi wowote, sisi na Watanzania wengi tunaompenda na kumuunga mkono tupo nyuma yake. Mwambie sisi Kanisa Halisi kila siku saa 11 alfajiri huwa tunaamka kumuombea mema kila siku, yeye na walio chini yake", akasema Baba Halisi kumwambia Waziri Masauni.
Mapema baada ya Waziri Msauni kufungua Ibada hiyo, Baba Halisi aliendesha Ibada ambayo iliambatana na kukusanya matunda (Sadaka) kwa ajili ya kumtolea Mungu Baba ili ayapokee mambi ya Ibada hiyo ya kuliombea Taifa liwe na amani na utulivu ambapo yeye na Mama Halisi walitoa sadaka ya familia kwa ajili ya maombi hayo.
"Tunapoomba hivi huku tukitoa matunda (sadaka) Mungu anapokea, siyo kwamba tunaiombea nchi amani kwa kuwa hakuna amani, hapana. sisi tunaomba amani na utulivu viendelee kuwepo ndiyo maana hata kama mvua inavyesha kuwa tunaomba inyeshe, ili iendelee kunyesha", alisema Baba Halisi.
Akizungumza wakati akifungua Ibada hiyo, Waziri Masauni alisema, Serikali inayoongozwa na Rais Samia itaendelea kuheshimu Uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Nchi, lakini akawataka viongozi wa Dini mbalimbali kuhakikisha wanazingatia wajibu wajibu wao wa kuongoza kwa mujibu wa sheria.
Masauni amewapongeza viongozi wa Dini kwa kuwa mstari wa mbele kuhimiza uadilifu miongoni mwa wananchi akisema uadilifu ukishamiri ndiyo inakuwa chachu ya amani na utulivu katika taifa lolote.
Amesema, hivi karibuni kumekuwepo na baadhi ya matukio ambayo yanaashiria kuporomoka kwa maadili na hofu ya Mungu, akitoa mfano kwamba tangu Januari Mosi hadi 15, mwaka huu, yametokea mauaji ya kifamilia na kwamba matukio hayo ni ishara ya kuporomoka kwa maadili hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuongeza bidhii katika kuwafanya wanajamii kuwa na hofu ya Mungu.
Masauni aliwapongeza Kanisa Halisi kwa kufanya Ibada hiyo na kusema kwamba viongozi wote wa dini wanapaswa kufanya hivyo.
Mkutano huo wa kuliombea Taifa Amani na Utulivu ambao ulihudhuria na watu wa aina mbalimbali, Uzao (Waumini) na Makuhani wa Kanisa hilo kutoka mikoani na baadhi ya Nchi za Nje, ulikuwa ni wa kuhitimisha Ibada ya siku 10 kwa ajili ya Matunda (Sadaka) kwa ajili hiyo ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu ambayo ilianza Januari 7, 2022 (3 Kiselu 1).
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Ndani Masauni Hamad Masauni Kalenda ya Majira na Wakati kabla ya uharibifu, wakati wa Ibada ya Kuliombea Taifa Amani na Utulivu iliyofanyika jana katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kalenda hiyo inayotumika kuhesabu majira hayo ambayo ni tofauti na Kalenda ya sasa ambayo mwezi wake wa kwanza unaanzia na Januari hadi Disemba, yenyewe kila mwezi una siku 28 na inaanzia mwezi Kisleu(1), Thebeti(2), Shebati(3), Adari(4),Abibu(5), Zivu(6), Siwani(7), Tamuzi(8), Abu(9), Eluli(10), Ethanimu(11) na Buli(12). (Picha na Bashir Nkoromo).
Post a Comment