Featured

    Featured Posts

MBUNGE LUGANGIRA AISHUKURU KAMATI KUU YA CCM KUMTEUA DK. TULIA KUWANIA USPIKA, ASEMA ANATOSHA

Dodoma, Tanzania
Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayewakilisha kundi la Asasi za Kiraia(NGOs) Tanzania Bara Neema Lugangira, ameipongeza Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpitisha Naibu Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson kugombea Uspika wa Bunge, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo, uliokamilika jana Jijini Dodoma.

Akizungumza Jijini Dodoma, Mbunge Neema Lugangira amesema, Kamati Kuu ya CCM chini ya Rais Samia imetumia hekima kubwa kwa kuwa kuchambua wanachama 70 wa CCM waliorejesha fomu za kuomba kuteuliwa na hatimaye kumteua Dk. Tulia aliyekuwa Naibu Spika kugombea Uspika.

Alisema jambo hilo ni kubwa sana na la kupongezwa kwa sababu kwanza limewapa imani kubwa wao kama Wabunge kuona kwamba namna gani Kamati Kuu ya CCM inathamini na kutambua uwezo wa Wabunge waliopo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nimefarijika sana kwamba mgombea wa nafasi ya Uspika kupitia CCM ametokea miongoni mwetu sisi Wabunge na naweza kusema Dk. Tulia nimemfahamu kutoka mwaka 2017 nilipopata bahati ya kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT kupitia Mkoa wa Kagera na kupitia Baraza hilo nikapitishwa kwa kura za kutosha katika Uchaguzi wetu nikawa Mjumbe wa Kamati ya Utekezaji UWT Taifa” Alisema Mbunge Neema Lugangira.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 kabla hajaingia kwenye Ubunge, Dk. Tulia amekuwa Mama hodari na shupavu ambaye amekuwa Mwalimu kwao na hata pale amekuwa akiona  mtu ana kitu ndani yake amekuwa mwepesi kuwa Mwalimu wa kujitolea.

“Nasema ule ualimu wake na jinsi alivyo hata ukiuliza Wajumbe wa Baraza la UWT wote wanafurahia uamuzi wa Kamati Kuu kupitisha jina la Tulia kugombea Uspika” Alisema Mbunge Neema Lugangira.

Mbunge Neema aliongezea kuwa amekuwa Mbunge kwa mara ya kwanza 2020 hadi sasa ni kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa na muda wote Dk. Tulia amekuwa Mwalimu na mwepesi kufikika na wakati wowote unaweza kutumia ujumbe akajibu na akakushauri.

Alisema pia hata wakati mwingine Mbunge yeyote anapokosea amekuwa akimwelekeza namna ya kuchangia wanapokuwa Bungeni kwa hiyo anaimani Kiti kimepata kiongozi hodari na shupavu.

Aidha alisema hata wakati akiwa Naibu Spika akiwa ameketi kwenye Kiti ameendesha Mijadala ndani ya Bunge kwa umahiri mkubwa sana huku akitoa uhuru wa kuchangia kwa kila Mbunge.

Mbunge Neema Lugangira alisema Dkt Tulia anauwezo na Kiti cha Spika na sio mara ya kwanza CCM kuteua Mgombea wa Uspika Mwanamke walishafanya hivyo kwa Mhe Mama Anna Makinda na hiyo inadhihiridha jinsi CCM ilivyokomaa Kisasia, Kidemokrasia na Haki Sawa za Kijinsia.

“Kwa mara nyengine napenda kuwashukuru Kamati Kuu ya Halmashuri kuu ya CCM kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha umoja na mshikamano baina yetu ndani ya Bunge kwa kitendo cha kuwarejeshea Dkt Tulia ambae ni Mbunge mwenzao. “Alisema

Alisema hiyo imewapa imani kubwa na hamasa zaidi ya yote kutokana na uwezo mkubwa na  hakuwezi kukatokea msukomsuko wa aina yote ile kwa sababu Dkt. Tulia  amekuwa Naibu Spika kwa Miaka Mitano na sasa kwa takribani Mwaka Mmoja na kidogo hivyo anajua namna kazi za Bunge zinavyoendeshwa, tulipofikia na nini kinapaswa kufuata.

Mbunge Neema Lugangira amesema Bunge litaendelea kuishauri Serikali kwa Uimara mkubwa huku akiweka wazi kuwa suala la Wabunge wenzake kumpigia kura za kishindo Dk. Tulia lipo wazi, watakwenda kukamilisha kazi iliyobakia maana Wabunge wote wameunga mkono na kwa kauli moja wanasema kwama Kamati Kuu ya CCM imefanya Maamuzi Sahihi.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) anayewakilisha Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Tanzamia Bara Neema Lugangira

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana