CCM Blog, leo
Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kushtushwa na ajali iliyotokea mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya watu 14 wakiwemo Waandishi 6 wa habari, mapema leo.
"Nimeshtushwa na vifo vya Watu 14 wakiwemo Wanahabari 6, vilivyotokea leo asubuhi baada ya gari lililokuwa katika msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kugongana Daladala. Poleni Wafiwa, Wanahabari na jamaa wote. Mungu aziweke mahali pema roho za Marehemu na Majeruhi wapone haraka,"ameeleza Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Ajali hiyo imehusisha magari mawili likiwemo la abiria aina ya Toyota Hiace na jingine lenye namba za usajili STK 8140 mali ya Serikali lililokuwa limebeba Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza wakitokea Mwanza mjini kwenda Ukerewe kupitia Bunda kushiriki ziara ya Mkuu wa mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel.
Kwa mujibu wa Taarifa rasmi za ajali hiyo Waandishi wa habari waliofariki ni Husna Milanzi wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Johari Shani wa Uhuru Digital, Antony Chuwa ambaye ni Mwandishi wa Kujitegemea, Afisa habari Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza Abel Ngapemba na Afisa Habari wa Wilaya ya Ukerewe Steven Msengi.
Taarifa hiyo imewataja waandishi waliojeruhiwa kuwa ni Mwandishi wa Kujitegemea Tunu Herman na Vany Charles wa Icon TV
Post a Comment