CCM Blog, Dodoma, leo
Rais Samia Suluhu Hassan, ameondoa kiwingu kuhusu hatma ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, baada ya kusema kuwa atakuwa nao kwenye ofisi yake.
Akizungumza leo, Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri , Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Rais Samia amesema Lukuvi na Profesa Kabudi amevuta ofisini kwake na atawapangia majukumu mengine.
Amesema Prof. Kabudi na Lukuvi wao amewaondoa katika Baraza la Mawaziri kwa sababu anataka awe nao katika ofisi yake kwa ajili ya kumsaidia katika kusimamia wengine walioko kwenye nafasi mbalimbali ambazo wameteuliwa na kuapishwa kuzitumikia.
"Hawamo katika Baraza la Mawaziri kwa sababu Lukuvi na Kabudi nimewavuta waje kwangu, ukiwangalia age (umri) wao ni kama wangu, na wale ambao nimewateua kule wengi ni vijana, hivyo tutashirikiana kusimamia wale ambao tumewapa nafasi. Waziri Kabudi amefanya kazi kubwa na nzuri ya kusimamia mazungumzo ya mikataba kati ya Serikali na Mashirika ya umma.
Hivyo huku kwangu pamoja na mambo mengine Profesa Kabudi atakuwa ndio Baba wa mikataba, Baba wa majadiliano na Lukuvi naye atakuwa pamoja na mimi, tunakwenda kuwasimamia ninyi(niliowateua). Lukuvi hatagombania Uspika, Lukuvi ametumikia Taifa hili kwa uadilifu mkubwa, hivyo tusimchafue", alisema Rais Samia na kuongeza;
"Nitakuwa naye katika ofisi yangu katika kuwasimamia wengine, ukiangalia umri wa Lukuvi na Kabudi wao wamebakisha mwaka mmoja , miaka miwili wastaafu, hivyo nitastaafu nao."amesema Rais Samia.
Post a Comment