Na Mwandishi Maalum
JUMUIA ya Wafanyabiashara Kariakoo, imemetuma salaamu za pole kwa wafanyabiashara wa Soko la Mchikichini kutokana kuteketea kwa moto soko hilo na kuwaomba wawe watulivu na kuamini serikali.
Pia imemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuyabadili matumizi baadhi ya maengo ya serikali yalioyowazi , Jijini Dar es Salaam, kuwa masoko ya biashara.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuhiya hiyo, Martin Mbwana, wakati akiongea na waandishi wa habari, Dar es Salaam, leo.
Amesema , baada ya makao makuu ya serikali kuhamia Dodoma, majengo mengi ya serikali mkoani Dar es Salam, yamebaki tupu ambapo serikali inaweza kuyageuza kuwa masoko maalumu ya biashara na kuingiza pato.
“Majengo tunayopendekeza yawe masoko ni Water Front, ambalo tunataka jengo zima liwe Soko Kuu la Vitenge,”ameeleza Mbwana.
Jengo lingine ni Ushirika ambalo wanapendekeza jengo zima liwe na maduka ya vifaa vya ngozi.
“Tunamuoba Rais Samia, atupe jengo la ushirika ili liwe soko kubwa la ngozi hapa nchini,”amesema Mbwana.
Jengo lingine ambalo jumuia hiyo imependekeza liwe soko kuu la vifaa vya kiletroniki ni Pamba House, lililopo katikati ya Jiji.
Ameeleza jengo hilo pia liwe soko la maduka yote ya simu na vifaa vyake.
“Serikali chini ya Rais Samia imefanya juhudi kubwa binafsi za kujenga masoko makubwa ya kisasa ambayo yanatumika na kuleta tija kubwa lakini ili kupanua wigo, ingalie pia majengo haya yaliyowazi kuyageuza masoko makubwa ya biashara,” amesema mwenyekiti huyo.
Ameeleza Jumuia ya Wafanyabiashara Kariakoo, inaimani kubwa na serikali katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo ujenzi wa majengo mawili ya kisasa ya Soko Kuu la Kariakoo na Soko Dogo la Kariakoo unaoendelea.
“Yakikamilika masoko haya Kariakoo itazidi kufunguka na kuwa kitivo cha biashara kama ilivyo kuwa awali. Rais wetu ametoa sh. bilioni 33 kwaajili ya ujenzi huo na kazi inaendelea,”amesema MBwana.
Kuhusu kuungua kwa Soko la Mchikichini, Mbwana ameeleza kuwa Jumuia ya Wafanyabiashara Kariakoo, imeguswa na hali hiyo na kuwapa pole wafanyabiashara wenzao.
“Kikubwa wafanyabiashara wa Mchikichini wawe wavumilivu, waiamini serikali kwani ni sikivu,”amesema.
Ameiomba serikali pia kuliangalia suala hilo kwa uzito kwani wafanyabishara hao wamepata hasara , ikiwemo kuwajengea soko la kisasa na lenye usalama kama yalivyo masoko ya Kisutu na Magomeni.
Akizungumzia hatua ya serikali kuwapanga wafanyabiashara wgo ‘Machinga’, Mbwana alisema, kumekuwa na tija kwani tangu Desemba mwaka jana, wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wameongezeka kutokana na kuamini usalama wa soko.
Post a Comment