Featured

    Featured Posts

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZITAKA TAASISI ZA FEDHA KUWEKA MASHARTI NAFUU YA MIKOPO YA KILIMO

Na Mwandishi Maalum, Katavi
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amezitaka Taasisi za Fedha nchini kuweka masharti nafuu ya mikopo kwa Wakulima ili waweze kukopesheka ili mikopo hiyo iwasaidie kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo katika Vijiji vya Isinde na Songambele vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkoani Katavi, wakati akizungumza na wakulima maeneo hayo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofadhiliwa na Shirika la Mageuzi ya Kijani Afrika (AGRA).

“Ni kweli masharti ya mikopo inayotolewa na Taasisi nyingi za fedha si rafiki kwa mkulima mdogo kukopesheka, ninafahamu kwamba Taasisi za fedha zinaongozwa na sheria ya Benki Kuu juu ya masharti ya mikopo, lakini ziangalie namna nzuri ya kuweka masharti nafuu kwa wakulima kukopesheka kirahisi pasipo kuathiri takwa la Benki Kuu.

Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya Taasisi za fedha kupunguza riba zao kwa mikopo ya kilimo na kwa sasa tumeanza kushuhudia Benki nyingi zikitoza riba isiyozidi asilimia10 kwenye mikopo ya Kilimo.
Hii ni hatua kubwa katika kuelekea kuwa riba ya tarakimu moja kwenye mikopo ya Kilimo hapa nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo,” Alisema Naibu Waziri Mavunde.

Alisema sanjari na mafanikio yaliyoanza kuonekana kwa Taasisi za Fedha kupunguza riba za mikopo, sasa ni imefika wakati ambao Taasisi hizo za fedha zitazame ambavyo zinaweza kufanya ili kulegeza masharti ya mikopo kwa walima hasa wadogo ili wakopesheke.

Mapema, mkulima Aniceth Gosberth na Muuzaji wa pembejeo za kilimo Eutropia Sangu, walimuomba Naibu Waziri Mavunde Serikali isaidie ili Taasisi za Fedha zilegeze masharti ya mikopo ili Wakulima wakopesheke kwa kuwa wanaamini wakipata mitaji zaidi wataweza kuimarisha kilimo na kuongeza tija.

Ziara hii inayoongozwa na Mjumbe wa Bodi ya AGRA na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, pamoja na Makamu wa Rais wa AGRA Aggy Konde, imehitimishwa leo baada ya kukagua miradi zaidi ya 20 katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.

Zaidi ya jumla ya wakulima, wauza pembejeo na wasindikaji 100,000 wamenufaika na ufadhili wa AGRA kupitia huduma mbalimbali.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akizungumza na Wakulima na Wananchi katika Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi. Picha zaidi, Bofya HAPA
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana