Na WyEST, MAFIA
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Mafia unakamilika Mei 31, 2022 kama ilivyopangwa.
Ameyasema hayo Machi 28, 2022 wilayani Mafia mkoani Pwani wakati alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya hiyo ambapo amesema jumla ya Shilingi bilioni 20 za ahueni ya Uviko 19 zimetolewa ili kukamilisha ujenzi wa vyuo 25 vya VETA vya Wilaya mbalimbali nchini.
"Ujenzi wa chuo hiki ulisimama baada ya fedha za awali Shilingi bilioni 1.6 kuisha, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea fedha za ahueni ya Uviko 19 ametoa zaidi ya Sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hiki," amefafanua Mhe. Kipanga.
Aidha ameutaka uongozi wa VETA kushirikiana na uongozi wa wilayani hapo katika kupendekeza aina ya mafunzo ya kutolewa chuoni hapo yanayoendana na shughuli za kijamii za wananchi wa Wilaya hiyo.
"Wilaya hii ina takribani jumla ya watu elfu 53, kati yao zaidi ya watu elfu 20 wanajihusisha na masuala ya uvuvi na wengine masuala ya utalii, hivyo ni muhimu sana kuwa na mafunzo hayo katika chuo hiki," amesema Naibu Waziri Kipanga.
Akiongea katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo amemuomba Mhe. Kipanga chuo hicho kitoe pia mafunzo yanayoendana na shughuli za kijamii za wilayani hapo.
"Shughuli kuu za kiuchumi Wilayani hapa ni uvuvi na utalii, hivyo tunaomba katika kozi zitakazotolewa chuoni hapa zisikosekane kozi za fani hizo," amesema Mhe. Ntembo.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa chuo hicho, Kaimu Mkuu wa Chuo, Harry Mmari amesema ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 70 na kwamba chuo hicho kitakuwa na jumla ya majengo 17.
Amesema chuo hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 720 kwa mwaka, kati yao 240 wa mafunzo ya muda mrefu ambao 144 kati yao watakaa bweni na 96 wa kutwa. Ameongeza kuwa wanafunzi wengine 480 watakuwa wa kozi za muda mfupi.
Post a Comment