Bungeni, Dodoma
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi ambao wameguswa na msiba kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM mkoa wa Rukwa Irene Nyamkama.
Amewasilisha salam hizo leo, alipokuwa akizungumza wakati wa tukio la kuagwa Bungeni Jijini Dodoma, mwili wa Marehemu Irene, ambapo aliungana na Wabunge na Waomboezaji mbaimbali akiwemo Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson.
Dk. Mpango amesema kila kiongozi anapaswa kujifunza na kuishi maisha ya uzalendo kwa Taifa kwa kutumikia vema nafasi anayopata kama alivyokuwa akifanya Irene Ndyamkama enzi za uhai wake na kuwaasa wabunge kujifunza yale mema aliyoyafanya mbunge huyo, ikiwemo kuwajali wale wanaoishi katika mazingira magumu kama vile yatima na wajane.
Akitoa salamu za rambirambi za serikali, Makamu wa Rais ameipa pole familia ya Marehemu Irene, Spika wa Bunge , Naibu Spika ,Wabunge pamoja na waombolezaji wote kufuatia kifo cha mbunge huyo na kuwaomba kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Kwa Upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema marehemu Irene alikuwa mfuatiliaji wa kazi zake kwa Mawaziri ili kuwasaidia wale anaowawakilisha Bungeni na kuwaasa wabunge kumuombea ili apumzike kwa amani pamoja na kumuenzi kwa kuendeleza yale mema alioyafanya katika utumishi wa Bunge.
Awali Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson alisema Marehemu Irene aliishi Maisha ya ukamilifu kwa kuishi vema na watu akisema mbunge huyo alijaaliwa utu, upendo na heshima hali inayofanya kumkumbuka wakati wote na kushukuru kwa maisha yake hapa duniani.
Baada ya kuagwa Bungeni leo, mwili wa marehemu Irene amefariki Dunia Aprili 24, 2022 katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha mkoa wa Pwani alikokuwa akipatiwa matibabu utapelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma, na kesho utasafirishwa kwenda Sumbawanga mkoani Rukwa ambako utaagwa kwa kufuata utaratibu utakaokuwa umeandaliwa na uongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge juzi, inataraajiwa mwili wa marehemu Irene utazikwa Aprili 29, 2022 Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, akizungumza wakati wa kuagwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM mkoa wa Katavi Irene Nyamkama, Bungeni Jijini Dodoma, leo.
Post a Comment