ARUSHA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameupongeza Mkoa wa Arusha chini ya uongozi wa Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kwa ubunifu wa kuanzisha karakana yenye uwezo wa kuzalisha nguzo 100 za majina ya barabara na mitaa kwa siku moja na ambazo zitarahisisha uwekaji wa miundombinu hiyo ya Mfumo wa Anwani za Makazi mkoani hapo.
Akiwa katika Mkoa wa Arusha tarehe 12 Aprili, 2022 Waziri Nape amefanikiwa kukagua miundombinu ya Anwani za Makazi, kupokea taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Mfumo wa Anwani za Makazi pamoja na kutembelea karakana hiyo iliyopo katika kata ya Kaloleni wilaya ya Arusha.
“Niwapongeze kwa kuanzisha karakana yenu wenyewe, huu ni ubunifu mkubwa na pia ni fursa na inapunguza gharama za utekelezaji wa operesheni ya mfumo wa Anwani za Makazi”, Amezungumza Nape
Aidha, amezungumzia faida za Mfumo wa Anwani za Makazi ambapo kwa Mkoa wa Arusha utasaidia kuongoza watalii kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kutumia programu tumizi ya Mfumo huo (NaPA) ambao utasaidia sana watalii kwa kuwa wataweza kuwasiliana na mfumo kuwapeleka mahali wanapotaka.
Ameongeza kuwa, “Tunaposema Mfumo wa Anwani za Makazi unaenda kuboresha ufikishaji wa huduma tunamaanisha tunaenda kuiingiza nchi ya Tanzania kwenye nchi zenye ustaarabu zinazohudumia wananchi wake pamoja na wageni kistaarabu”.
Katika hatua nyingine Waziri Nape amewaomba viongozi wa dini mbalimbali kumuunga mkono Mhe. Rais katika operesheni hii kwa kutoa elimu kwa waumini wao juu ya manufaa, umuhimu na fursa zinazopatikana kupitia Mfumo wa Anwani za Makazi
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amesema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaelekeza zoezi hili kukamilika ifikapo 22 Mei, mwaka huu lakini kwa mkoa wa Arusha wamejipanga kukamilisha ifikapo tarehe 30 Aprili, 2022 kwa kuwa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga kusimamia utekelezaji katika halmashauri zote saba za mkoa huo na wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amepongeza ubunifu wa mkoa wa Arusha katika kutekeleza operesheni ya Mfumo huo, aidha ametoa taarifa ya Mfumo wa NaPA unaotumika kuingiza taarifa za makazi na wakazi tayari umewekewa namba ya usaidizi muda wowote inapotokea changamoto
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwa Waziri Nape utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi kwa jiji la Arusha ni asilimia 78.7, kwa mchanganuo wa Halmashauri ya Monduli asilimia 45.82, Ngorongoro asilimia 12.51, Arusha DC asilimia 11.21, Meru DC asilimia4.2, Karatu DC asilimia 2.59 na Longido Dc asilimia 39.04.
Post a Comment