Featured

    Featured Posts

'MTANZANIA' KUTOKA SAME MKOANI KILIMANJARO ASHINDA KITI CHA UDIWANI NCHINI UINGEREZA

Dar es Salaam.
Raia wa Uingereza mwenye asili ya Tanzania, Linda Lusingu ameshinda Kiti cha Udiwani Kata ya East Barnet, katika mji Mkuu wa London kwa kuwashinda wagombea wenzake 10, akipeperusha bendera ya chama cha Labour katika uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.

Ushindi wa Lusingu ambaye ni mtaalamu wa sheria za familia na watoto, umechangia chama hicho cha Labou kujipatia madiwani wengi katika Halmashauri ya Kata ya Barnet iliyokuwa ikiongozwa na chama cha Conservative kwa miaka mingi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam na baadaye na gazeti moja la kila siku hapa nchini, Lusingu ambaye ni mwenyeji wa Same, Kilimanjaro, alisema amekuwa mwanachama wa Labour kwa miaka 13 na kwake imekuwa safari ndefu hadi kushinda nafasi hiyo.

“Haikuwa rahisi kufikia hapa, hasa ukichukulia kuwa natoka kwenye jamii za watu weusi wachache ambao hawana uwakilishi, sikuzaliwa huku na siyo mtu mweupe, kwa hiyo kuna ubaguzi mwingi.

“Nilienda Uingereza nikiwa na umri wa miaka 15 na nimeishi kwa miaka 23. Niliingia kwenye mambo ya siasa karibu miaka 13 iliyopita baada ya kumaliza masomo ya chuo na nikapata nafasi ya kufanya kazi kwa mbunge sehemu niliyokuwa nakaa na huo ndio ukawa mwanzo wa safari hii,” alisema Lusingu.

Alisema kwa kipindi hicho alifanya naye kazi na kuona anavyofanya na kusaidia watu kwenye jamii, kama yeye alivyofika huko akiwa na mambo mengi yaliyohitaji msaada wake ikiwemo viza, nyumba na mambo mengine ambayo kama wageni wangehitaji.

“Aliponipa hiyo nafasi nikaona ni nafasi nzuri na nikaendelea kuwa kwenye chama na ilipokuja hiyo nafasi nikaamua kuwania,” alisema.

Alieleza kuwa kama wanachama wa Labour walifanya kazi sana kwa kuongea na wakazi wa eneo hilo kuhusu shida zao, hasa ugumu wa maisha, gharama za kuishi na kutofurahia mambo yaliyofanywa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Borris Johnson kama marufuku ya kufungia watu (lockdown) wakati wa Uviko-19.

“Watu walipoteza ndugu zao kipindi hicho ingawa yeye alikuwa akifanya sherehe, na sheria alizoziweka alikuwa hazifuati, hicho kiliumiza watu wengi na hiyo ilitusaidia kidogo kushinda.

“Lakini la muhimu ni kwamba tulifanya kazi na kuongea nao, lakini tuliwapa ilani ambayo wao waliamua kutuunga mkono na ndiyo maana tumeshinda.”

Licha ya Serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo kufanya vibaya kwenye uchaguzi huo, anaamini ushindi wa Labour umetokana na sera na ilani aliyosema ilileta matumaini kwa wananchi waliokata tamaa. 

 

Alisema alikwenda Uingereza wakati baba yake akisoma huko na yeye kusomea huko. Kwa sasa baba yake amesharudi Tanzania.

Linda Lusingu
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana