Arusha, Tanzania
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino amesema Shirikisho hilo linaridhishwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo, hivyo litaendelea kuisaidia Tanzania.
Rais Infantino amesema hayo usiku wa kuamkia leo Agosti 10, 2022, baada ya kuwasili hapa nchini na kupokelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro akiongozana na wachezaji mahiri wa zamani waliopata kucheza katika makombe ya Dunia na Mwamuzi Corina.
Katika mapokezi ya Rais huyo wa FIFA, Waziri Mchengerwa amesema kuwa Shirikisho hilo la FIFA limekwishatoa msaada wa ujenzi wa viwanja changamani Dar es Salaam na Tanga lakini wako tayari kwa ajili ya kuongeza vituo katika Kanda nyingine, na kumshukuru Rais Samia kwa jitihada kubwa ambazo zimesaidia Tanzania kupiga hatua duniani katika michezo.
Rais huyo wa FIFA na viongozi mbalimbali wa juu kwenye Soka Dduniani wamewasili nchini kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) unaofanyika leo jijini Arusha unaotarajiwa kuhudhuria na zaidi ya watu 500 na waandishi wa habari zaidi ya 100 huku ikitarajiwa kuangaliwa kupitia mawasiliano mbalimbali na zaidi ya watu Bilioni moja Duniani.
Tayari viongozi wakuu wa mashirikisho yote ya Soka kutoka mabara yote Duniani wamewasili na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa anatarajiwa kumwakilisha Rais Samia kwenye mkutano huo ambao ni wa Kihistoria katika medani ya soka kuwahi kufanyika Tanzania.







Post a Comment