Na Rosena Suka, Lushoto
Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana Agosti 9, 2022 alifungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Mahsusi wapatao 56 wa Mahakama ya Tanzania yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa Ofisi.
Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Mafunzo uliopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Makatibu Muhtasi kutoa huduma bora zinazoendana na uwekezaji katika majengo ya Mahakama nchini.
Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, aliendelea kwa kusema kuwa, Mahakamaya Tanzania iko katika maboresho ambayo yanagusa maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na raslimaliwatu hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa watumishi hao ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea.
“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.
Mhe. Dkt. Kihwelo aliwasihi watumishi hao kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuipa sifa nzuri Mahakama ya Tanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua Mahakama kama matumizi ya lugha mbaya na kuwaomba watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi kushirikiana na kuonyesha waliochojifunza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali ili kuendana na maboresho yanayoendelea.
Bi. Beatrice Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, washiriki sita wakiwa ni waajiriwa wapya.
Amesema, watumishi hao wanapewa mafunzo hayo kwa lengo la uwakumbusha majukumu yao ya kazi za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi, uzalendo na protokali na mipango ya Mahakama.
Uboreshaji, huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na ushauri, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika leo tarehe 9 Agosti, 2022.
Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.

Post a Comment