Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kinondoni Anna Hangaya au Mama Makete amefanikiwa kutwaa tena nafasi hiyo, baada ya kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa Jumuiya hiyo uliofanyika jana Msasani jijini Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kigamboni Stanley Mkandawile alisema Mama Makete ameshinda kwa kupata kura194 kati ya kura zote 344 zilizopigwa.
Mkandawile alisema, Lilian Mchaa aliyekuwa akijaribu kumfurukuzia Mama Makete, aliambulia kura 146 katika kinyang'anyiro hicho ambacho wagombea Uenyekiti walikuwa wanne.
Akizungumza baada ya matokeo, Mama Makete amesema "Namshukuru Mungu kuniwezesha kushinda na kuwa mwenyekiti tena wa Jumuiya yetu Wilaya ya Kinondoni. Nawashukuru wote tuliokuwa tunashindana katika nafasi hii. Sasa uchaguzi umekwisha nawaomba tuendelee kuwa kitu kimoja".
"Baada ya uchaguzi huu, kilichobaki sasa tujipange na tuweke nguvu zetu pamoja kuhakikisha 2025 tunampitisha kwa kishindo Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama", alisema Mama Hangaya.
Akizungumza baada ya kutangaza matokeo, Mkandawile aliwataka UWT Kinondoni wote kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan ili juhudi zake za kuiletea Tanzania maendeleo zizidi kufanikiwa.
" Kwa bahati nzuri ninyi Kinamama mmebahatika kuwa na mwanamke mwenzenu ambaye ni mfano bora wa uongozi, mtu makini na mchapakazi, hivyo naamini mtafuata nyayo zake na kuwa naye bega kwa bega ili azma yake ya kuivusha mbali zaidi Tanzania kiuchumi na kidiplomasia izidi kupata mafanikio", alisema Mkandawile.
Nafasi nyingine zilizokuwa zinapambaniwa katika Uchaguzi huo ni Uwakilishi wa Vijana ambapo alishinda Mariam Mziwanda wa Kampuni ya Uhuru Publications (Ltd) akiwabwaga Lilian Rewbangira na Cecilia Jeremia, huku Mkutano Mkuu akishinda Kuruthumu Segamiko, Salama Chaurembo Halmashauri Kuu na Jenifa Barongo akasinda kwenda Jumuiya ya Wazi.
Aidha ulikuwepo pia mchuano mkali kwenye nafasi ya Baraza Kuu la UWT wilaya hiyo ya Kinondoni ambapo ni wanane tu waliofanikiwa kupenya kati ya jumla ya Wagombea 24 waliokuwa wanawania nafasi hiyo na aliyeongoza kwa kura kati ya walioshinda ni Stella Walingozi.
Post a Comment