Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Kuna kisa kimoja ambacho nilisimuliwa na Ndugu mmoja ambaye hapa sitamtaja, lakini ni mtu mwenye hekima sana. Huyu ukizungumza naye japo kwa muda mdogo, utaachana naye ukiwa umepata mawili au matatu ya hekima kutoka kwake.
Siku moja katika mazungumzo na Ndugu huyo, tukagusia hatma ya maisha ya sisi binaadamu hapa duniani. Yule Ndugu akasema "Ndugu yangu kifo ni siri ya Mungu Baba peke yake, analeta kiumbe chake duniani bila chenyewe kujua na hali kadhalika hubakia ni siri yake siku na saa ya kukichukua hicho kiumbe chake".
"Ngoja nikusimulie kisa hiki", akasema huyo Ndugu, kisha akaanza kusimulia akisema; "Wikendi moja marafiki walikutana wakanunua mbuzi kisha wakamchinja na kupikiwa supu mahala hapo walipokutana. Supu ilipokuwa tayari kila mmoja akajaza kwenye chombo supu tele, wakaanza kula huku wanapiga soga.
Wakati wakiendelea kula supu, mmoja kati yao akawaambia wenzake, "najisikia kwenda haja, hebu nifunikieni supu yangu naenda msalani, nitakuja kuendelea", baada ya kuondoka kwenda msalani wenzake wakaendelea kula supu hata wakawa wametosheka, ikawa wamebaki kumsubiri yeye tu atoke msalani.
Watu wale walimsubiri wee! wakatahamaki nusu saa nzima imepita, wakaamua kwenda kumuangaalia huko mslani, Lahaula! walipoingia msalani wakakuta mwenzao alishafariki muda mrefu, ni nzi tu ndiyo wame 'mpamba' mdomoni na mapuani! Wakaangua kilio kilichochanganyika na butwaa! Naam, amekwisha lala usingizi wa milele!". Basi hivyo ndivyo maisha yalivyo.
Bila shaka waliokaribu na masuala ya Siasa na Burudani hasa ya nyimbo za kwaya, hivi sasa ninapowatajia jina la aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge na Mkurugenzi wa Kikundi cha Tanzania One Thetre (TOT) Hayati Kapteni John Komba lazima mwili utawasisimka kwa kukumbuka kiumbe huyu alivyokuwa mahiri katika uimbaji na katika siasa.
Alifanya kazi zake kwa juhudi na maarifa na kwa weledi mkubwa, na bila shaka aliwasidia wengi kuinuka kimaisha na pia kuinuka kisiasa. Lakini tazama japo sote tunajua kwamba kifo kipo, hakuna aliyeweza kujua kwamba Kapteni Komba angeiaga dunia lini na kurejea kwa Mungu Baba.
Sasa ni miaka 7 na miezi kadhaa tangu Kapteni Komba alipoiaga Dunia Feabruari 28, 2015, na bila shaka bado anakumbukwa na wengi.
Hivi majuzi nilipokuwa nyumbani kwa familia iliyoachwa na Kapteni Komba, Mbezi Beach Kwa Komba, Kawe Jijini Dar es Salaam, nikapata kuzungumza mawili au matatu na Mjane Salome John Komba, katika mazungumzo hayo akatoa kitabu kimoja na kunionyesha akisema "Mwanangu unakiona kitabu hiki, kina historia yote ya rafiki yako Kapteni Komba".
Baada ya kukipokea na kukisoma ukurasa kwa ukurasa nikakubaliana na Bi Salome, Mjane wa Kapteni Komba, kwa kweli kitabu hicho kimesheheni historia ya kutosha ya hayati John Komba maana kinaeleza tangu kuzaliwa kwake hadi maziko yake. Kitabu chenyewe hicho hapo
Post a Comment