Na WyEST,
DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) Septemba 5, 2022 ameitambulisha rasmi kwa Bodi na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) timu itakayofanya mapitio ya utaratibu wa utoaji mikopo kwa miaka mitano iliyopita ili kuona namna ya kuboresho utaratibu huo.
Amefanya utambulisho huo jijini Dar es Salaam ambapo ameongeza kuwa timu hiyo pia itaangalia taarifa ambazo zimekuwa zikitumika kuomba mikopo kwa kipindi hicho ili kuona iwapo zinatosheleza au kutahitajika taarifa za ziada ili kuboresha zoezi hilo na kuipa timu hiyo mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo.
Profesa Mkenda amewataja wajumbe wa timu hiyo kuwa ni Prof. Allen Mushi, Dkt. Martin Chegere na Iddi Makame na kuongeza kuwa wajumbe hao wote ni wataalamu ambao ana imani kuwa watafanya kazi kwa weledi na umakini wa hali ya juu.
"Lengo kuu la kufanya mapitio haya ni kuhakikisha tunaboresha zoezi la utoaji mikopo na kuhakikisha inatolewa kwa haki na kufuata vigezo vilivyotangazwa ili kupunguza au kumaliza kabisa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza," amefafanua Prof. Mkenda.
Wakati huo huo, Waziri Mkenda amewataka wanafunzi watakaoomba mikopo kuhakikisha wanatoa taarifa kamili na sahihi ili kuepusha kukosa kwa wanafunzi wanaostahili.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya HESLB, Prof. Hamisi Dihenga amesema Bodi itashirikiana na timu hiyo ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa mafanikio.
Naye Prof. Mushi akiongea kwa niaba ya timu hiyo ameishukuru Wizara kwa kuwa na imani nao na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na uaminifu.
Post a Comment