Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Serikali ya Tanzania imetanga msamaha wa kutokushitakiwa kwa mtu yeyote ambaye atasalimisha silaha anayoimiliki isivyohalali na kwamba usalimishaji huo utafanyika katika vituo vya Polisi, ofisi za serikali za mitaa au vijiji na kwamba mtu yeyote atakayepatikana na silaha haramu baada ya muda huo wa msamaha kupita atachukuliwa hatua kama mhalifu mwingine.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa mwezi wa msamaha wa usalimishaji silaha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amesema kuwa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataendesha kampeni maalum ambayo itashirikisha kamati za usalama za mikoa na wilaya, taasisi za kidini, vyombo vya habari na wadau wengine.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema kuwa, hakuna mtu yeyote atakayechukuliwa hatua za kisheria atakaposalimisha silaha kwa hiari katika kipindi kilichotolewa kuanzia tarehe 01 Septemba 2022 hadi 31 Oktoba 2022 na kwamba mtu atakayepatikana na silaha anayoimiliki kwa njia ya haramu baada ya muda huo atachukuliwa hatua za kisheria.
IGP Wambura amewataka pia wanaomiliki silaha kihalali kuzingatia sheria na kanuni zilizopo ili silaha hizo zisiangukie kwenye mikono ya wahalifu.
Post a Comment