Na Mashaka Mhando, Tanga
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, Henry Daffa Shekifu, amesema angetamani wachaguliwe tena katika uchaguzi wa chama ili wakapate fursa ya kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Aidha, Shekifu amesema endapo atachaguliwa tena, mkoa wa Tanga utakwenda kumpa zawadi Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kutokana na kazi nzuri anazofanya nchini.
Akizungumza katika mkutano wa mwisho wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tanga, Shekifu alisema ampongeza Rais kwa kazi anazozifanya na wanataka aendelee na Urais mwaka 2025.
"Nampongeza Rais wetu huyu ni mtu wa Tanga hasa, amekuwa na mapenzi ya mkoa wetu naamini mwaka 2025 hatuna zawadi nyingine ya kumpa Mwenyekiti wetu zaidi ya kumtaka aendelee na uongozi kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa mkoa wetu," alisema Shekifu na kuongeza,.
"Nawaasa wale wenzetu watakaochaguliwa na mimi nikiwemo, kama nitachaguliwa na tukishachaguliwa, wote twende upande mmoja wa kuheshimu kazi alizozifanya Mwenyekiti wetu na anazoendela kuzifanya,".
Alisema anaomba mungu wenzake walioomba nafasi mbalimbali katika chama na jumuiya za chama hicho, waweze kuchaguliwa tena ili waweze kusimamia kazi za Maendeleo ya mkoa huo ikiwemo kusimamia ilani ya chama.
"Tuombe mungu ningependa turudi wote, na namuomba mungu aturudishe wote sijafanya dhambi kwa kusema haya hizo sifa na utendaji wenu ndiyo unaonifanya niseme tubaki wote na hata wenzangu pia mngetami tubaki wote Kwasababu Maendeleo tuliyoyapata ni dhahiri na siyo ya kubuni," alisema Shekifu.
Hata hivyo, aliwaasa watakaochaguliwa katika uchaguzi huo wahakikishe wanakuwa waadilifu, wenye kufuata taratibu, kanuni na katiba ya CCM.
Shekifu aliwashukuru viongozi mbalimbali ambao amshirikiana nao katika uongozi wao unaomalizika mwaka huu na akataka watakaochaguliwa waendeleze ushirikiano kwasababu mkoa wa Tanga una heshima kubwa ndani na nje ya mkoa huo na mikoa mingine imekuwa ikijifunza kutoka mkoa huo.
Awali akitoa salamu katika mkoa huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutokea mkoa huo MNEC Mohamed Salimu maarufu kwa jina la Ratco, alisema watakaoshindwa kuchaguliwa katika chaguzi za chama zinazoanza wiki ijayo ngazi ya jumuiya, wilaya na mkoa wasofanye nongwa, washirikiane na wenzao watakaochagauliwa ili kikijenga chama hicho.
"Tusijenge chuki kama mtu kura hazitatosha tuache nongwa, tushirikiane kukijenga chama chetu, mtu ukifanya nongwa haitakusaidia maana chaguzi zetu zinaendeshwa kwa haki," alisema MNEC.
Katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Suleiman Mzee Suleiman alisema majina watakayoyarejesha kupigiwa kura wameyachunja na kuchambua kwa umakini mkubwa tangu walipoanza kupokea majina Julai 2 mwaka huu walipoanza kutoa fomu kwa wagombea.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Henrry Shekifu
Post a Comment