Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabuka amewataka wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri sambamba na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati.
Dkt Mabula alisema hayo wilayani Kibaha tarehe 1 Sept 2022 wakati alipokwenda na Waziri wa Uvuvi na Mifugo Mashimba Ndaki kupokea na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika eneo la kiwanja namba 34 Pangani Kibaha chenye ukubwa wa hekta 1037 ambapo wananchi 1002 wamebainika kuvamia kiwanja cha eneo hilo linalomilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya taasisi yake TVLA ,
Katika uchunguzi wake, Kamati ilifanikiwa kuwahoji wananchi wavamizi 1,156 katika
mitaa ya Kidimu, Lumumba na Mkombozi na kuwasikiliza, kuwahoji na kupokea vielelezo mbalimbali kutoka kwa wananchi wavamizi 1002 ambapo wavamizi 154 hawakuwa na nyaraka zozote za namna walivyopata maeneo kwenye eneo hilo.
Akisoma taarifa ya Kamati ya uchunguzi, Katibu wa Kamati ambaye ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Pwani Husein Sadick, alisema katika mahojiano na wananchi hao, 403 walikiri kuvamia kwa kujikatia vipande vya ardhi, 46 walidai kupewa vipande vya ardhi na wavamizi waliotangulia na wananchi 6 walidai walirithi maeneo hayo. Hata hivyo, wavamizi hao wamefanya maendelezo pasipo kupata kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri kama taratibu zinavyoelekeza.
Kwa mujibu wa Husein Sadick, historia ya eneo hilo ilianza 1982 kwa Wizara kuomba eneo la kuzalisha mitamba kwa ajili ya kuhudumia kanda ya mashariki na hekta 4000 kutwaliwa huku wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo walilipwa fidia kwa awamu tofauti.
"Eneo lilipatikana kihalali na wizara na mwaka 2007 wananchi walivamia ambapo tathmini ya kamati ilibaini uwepo nyumba zilizojengwa kwa tope au mabati, nyumba zisizokamilika au chumba kimoja pamoja na zile zenye makazi" alisema Husein Sadick
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Lumumba kata ya pangani Kibaha mkoani Pwani Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitoa rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati.
‘’Nitoe rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati’’ alisema Dkt Mabula
Akielezea mgogoro katika eneo la Pangani, Waziri wa Ardhi alieleza kuwa, katika eneo hilo ilibainika uwepo wa wavamizi waliounda magenge ya kutapeli wageni kutoka nje ya Kibaha hasa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na kujifanya wamiliki wa asili katika maeneo waliyovamia.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alielekeza wananchi wote waliouziwa ardhi ndani ya Kiwanja Na. 34 Pangani kuwafungulia mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wale wote waliowauzia ardhi pamoja na walioshirikiana nao kufanya mauzo hayo.
Pia alitaka wavamizi wote waliotumia/kuandaa nyaraka za kughushi wachukuliwe hatua za kisheria kwa kusababisha uvamizi kwenye maeneo yenye miliki za watu wengine.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema, amefurahi mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na taasisi iliyo chini ya wizara yake mefikia mwisho na kuishukuru wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuunda tume ya kuchunguza suala hili.
"Naipongeza timu ya uchunguzi kwa kueleza ukweli na ukweli unapendwa na watu wachache na nakubaliana na mapendekezo yote ya timu ya uchunguzi" alisema Ndaki.
Ndaki alisema, Wizara yake ina huruma sana maana pamoja na kumiliki kihalali helta zote 4000 lakini bado imeamua hekta 2,963 kati ya hizo ziende halmashauri na wao kubaki na hekta 1,137.
Hata hivyo, Ndaki aliagiza kuchukuliwa hatua kwa yeyote atakayevamia tena eneo lililobaki huku akisisitiza mipaka ya eneo lililobaki ianishwe na kulindwa ili kuepuka uvamizi mwingine.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaji Abuubakar Kunenge alisema, uongozi wa mkoa wake utasimamia na kutenda haki wakati wa utekelezaji mapendekezo ya tume ya uchunguzi na kusisitiza haki itendeka.
"Katika kushughulikia utekelezaji mapendekezo ya kamati haki itatendeka na anayestahili watamlinda na asiyestahili atupishe na hakuna atakayenyang'anywa haki yake" alisema Kunenge.
Mkoa wa Pwani umekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambapo Waziri wa Ardhi aliunda Kamati ya Uchunguzi kubaini namna wavamizi walivyopata ardhi, kubaini matapeli wote waliohusika kuuza ardhi na kisha kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukua.
Post a Comment