Featured

    Featured Posts

MKAPA FOUNDATION YAISHAURI KAMATI YA BUNGE IUNDWE KAMISHENI HURU KUSIMAMIA BIMA YA AFYA KWA WOTE+video


Taasisi ya Benjamini William Mkapa Foundation imeshauri uwepo wa Kamisheni Huru ya kupitia gharama za huduma za Afya ikiwa ni pamoja na gharama za dawa, vifaa tiba, vitendanishi, na gharama za uendeshaji wa huduma, kama mishahara ya watumishi na tozo mbali mbali zilizo katika sekta ya Afya hapa nchini. Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Programu za Uboreshaji wa Huduma za Afya wa Taasisi hiyo, Hendrey Samky (pichani juu) walipokaribishwa wadau kutoa maoni yao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu uboreshaji wa muswada wa Bima ya Afya kwa Wote kwenye Ukumbi wa Bunge Dodoma Oktoba 19, 2022.


Samky akiwa na mtumishi mwenzie
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo akiongoza mkutano huo wa wadau.

Baadhi ya viongozi wa dini wakishiriki katika mkutano huo

Baadhi ya wadau waliohudhuria kutoa maoni yao kuhusu muswada wa Bima ya Afya kwa Wote.



Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.







 
Afisa Habari wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Grace Kisinga (kusto) akiwa na Afisa Habari wa Wizara ya Afya, Catherine Sungura wakifuatilia kwa makini maoni ya wadau.

 PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA

Mdau, nakuomba uendelee kusikiliza kupitia clip hii ya video, Hendrey Msamky akitoa maoni hayo kwa niaba ya Taasisi......



MAONI ,USHAURI NA MAPENDEKEZO

UTANGULIZI

 Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikifanya jitihada za kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi wote itakayowezesha kila mwananchi kupata huduma bora za Afya bila kukwama au kutumbukia katika dimbwi la umaskini kutokana na gharama za huduma za Afya. 

 Kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa Afya wa Tano (2021 – 2026), kiwango cha bajeti kilichowekwa kwa kila mwananchi kwa ajili ya kugharamia huduma za Afya kilishuka toka Tshs 44,549 kwa mwaka 2015/16 mpaka Tshs 42,147 kwa mwaka 2020/21. 

Pamoja na kiwango hiki kushuka bado kipo chini ya mapendekezo ya Shirika la Afya duniani la bajeti ya huduma za afya kwa mwanachi ya Dola za Marekani $86 – $122 (Tshs 199,812.4 – 260,220.8) ili kuwezesha kufikia adhma ya Afya kwa Wote (UHC). 

 Kwa sasa ni asilimia 15% tu ya Watanzania wana Bima ya Afya, jambo ambalo linaweka asilimia 85% ya watanzania katika matumizi ya fedha za papo kwa papo kuhudumia gharama za Afya, na hii ni changamoto kubwa kwa ustawi wa wananchi na Taifa.

 Hivyo basi, mwenendo wa Serikali kuanzisha Bima ya Afya kwa wote nchini, ni mwenendo wenye tija na wenye lengo zuri la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya afya bila maudhi au kipingamizi.

 Tunawapongeza Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na kupitia Wizara ya Afya chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, kwa maamuzi haya ya kuwasilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa wote Bungeni. 

 Taasisi ya Mkapa Foundation ambayo ni Taasisi ya kitaifa na muasisi wake na Hayati Benjamin William Mkapa na iliyojikita katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya nchini, inapenda kuwasilisha mapendekezo yafuatayo yatakayo boresha zaidi uandaaji na utekelezaji wa Sheria hii. 

 Maoni ya Ujumla kutoka Taasisi ya Mkapa: Ili Skimu za Bima ya Afya ziweze kuwa na uwezo wa kutoa huduma za Afya ni lazima kwanza kuwe na ufahamu wa gharama za huduma za Afya kwa kila tatizo la kiafya, ili gharama za kulipa skimu ziwe za uhalisia. 

Ili kufikia adhma hii, Taasisi inashauri uwepo wa Kamisheni Huru ya kupitia gharama za huduma za Afya ikiwa ni pamoja na gharama za dawa, vifaa tiba, vitendanishi, na gharama za uendeshaji wa huduma, kama mishahara ya watumishi na tozo mbali mbali zilizo katika sekta ya Afya hapa nchini. Bima ya Afya kwa wote ni muhimu iwe na gharama za uchangiaji halisi kutokana na mahitaji ya sasa. 

Aidha kwa sasa michango ya wananchi pekee haitaweza kuchangia gharama za Afya kutokana na hali zao za kiuchumi. Tunapendekeza mfumo wa uchangiaji uwe mfumo wa kikodi, kama ilivyo nchi ya Ghana, ambapo Seikali itachangia kwa kiwango kikubwa cha eneo la bima, na wananchi watachangia sehemu tu ya gharama ya Bima hiyo.

 Kama tulivyopendekeza katika eneo la Kitita cha Mafao ya Msingi (Kifungu15(1&3)), kutokana na uhitaji wa huduma za Afya kutofautiana kati ya mtu na mtu, ni muhimu skimu ziweke vitita vya mafao kadhaa vitakavyo toa tathmini ya kiwango cha uchangiaji kama ilivyo sasa kwa Bima ya Afya ya Taifa. 

Vitita hivi vitatoa uhuru kwa mchangiaji kuamua aina ya kitita anachokitaka, huku akiwa na uhakika wa kitita cha mafao ya msingi. 

Mfano mzuri pia ni nchi ya Rwanda yenye mfumo wa vitita vya mafao kadhaa vinavyo muwezesha mchangiaji kupata vitita kadhaa. Masharti yaliyowekwa kwenye Mswada huu yanagusa Sera, Miongozo, Kanuni na Waraka kadhaa zinazosimamia huduma za Afya hapa nchini haswa huduma za Mama na Mtoto, Wazee na huduma nyingine zinazofaidika na miradi msonge hapa nchini. 

Taasisi inapendekeza Sheria hii kuweka masharti ya kupitia miongozo hiyo na sera hizo, ili ziendane na masharti ya sheria hii mpya ya huduma za Afya kwa wote, hasa zile zinazogusa eneo la utoaji wa “huduma bure” ( bila malipo) kwa baadhi ya makundi yaliyo ainishwa hapo juu. 

 Utekelezaji wa Sheria hii utategemea kwa kiwango kikubwa ushiriki wa sekta binafsi kutokana na kiwango kikubwa cha mchango wao katika utoaji wa huduma za Afya hapa nchini, haswa katika Hospitali za Rufaa.

 Tunapendekeza, marekebisho ya mipango ya ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP), ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa sheria hii na kuepusha usumbufu wowote wakati wa utekelezaji kwa wananchi.

 Sheria kwa ujumla wake haijatambua mchango wa wadau mbali mbali wa sekta ya Afya nchini katika kuwezesha utekelezaji wake. 

Taasisi inashauri sheria iweke masharti ya kushirikisha wadau wa Afya katika majukumu yaliyo pewa Waziri katika sheria hii. Ubora wa huduma za Afya katika utoaji wa huduma kwa kila mwanachi ambae atakuwa na bima ya afya ni muhimu sana katika kuvutia au kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya. 

Maboresho haya hayana budi kujikita katika kuhakikisha wapo watumishi wenye stadi na weledi na wa kutosha kwa idadi. Hivyo tunapendekeza vituo vya tiba vya serikali na vya binafsi kuongeza idadi ya watumishi sambamba na uwepo wa dawa na vifaa Pamoja na miundombinu bora.

 Maoni Mahsusi Kifungu cha Mswada Eneo la Mswada Mapendekezo 3 Tafsiri – Mtegemezi maana yake ni (Uk. 7) Iongezwe tafsisri inayomhusisha mwenza wa mwanachama kama ilivyoa ainishwa katika kifungu Na.19 (Uk. 13) wa Mswada huu. 

Hivyo tasfiri zitaongezeka kuwa 4. 3 Tafsiri – Mtegemezi maana yake ni (Uk. 8) Sehemu ya C ya tafsiri inayomtaja ndugu wa damu inahitaji marekebisho kidogo kuweka maana/tafsiri ya neno “ndugu wa damu” (Mfano kaka, dada, mdogo/kaka/dada wa mwenza waliozaliwa na baba au mama mmoja) 7 (2)(e) Udhibiti wa mfumo wa bima ya Afya (Uk.9-10) (e)kutoa miongozo ya malipo kwa watoa huduma Sekta ya utoaji wa huduma ya Afya nchini ni eneo lenye wadau wengi huku sekta binafsi ikiwa na mchango mkubwa wa zaidi ya asilimia 30%.

 Ghrama za matibabu zinatofautiana kulingana taasisi inayotoa huduma na eneo la utoaji wa huduma.

 Kutokana na hili tunashauri sheria hii ianzishe chombo (commission) huru kitakachokuwa kinafanya tathimini ya gharama za huduma za afya nchini kwa watoa huduma mbali mbali na kutoa mapendekezo sahihi kwa Wizara ya Afya ili kuelekeza gharama za malipo kwa watoaji wa huduma kupitia Mamlaka inayotajwa na Sheria hii.

 14 (2) Vitita vya Mafao(Uk.12) Kitita cha mafao ya msingi kitatumika …..tangu tarehe ambayo mwanachama atasajiliwa…… Kifungu hiki kirekebishwe na kisomeke; “Kitita cha mafao ya msingi kitatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja na mwezi mmoja tangu tarehe ambayo mwanachama atasajiliwa kujiunga na Bima ya Afya kwa mara ya kwanza na mara moja kabla ya kuhuisha uanachama”.

 15 (1) Kitita cha mafao ya msingi (Uk.12) Tunashauri kifungu hiki kiainishe mafao ya msingi atakayonufaika nayo mwanachama ili kuyapa ulinzi wa kisheria. 15 (3) Kitita cha Mafao ya Msingi (Uk.12) Tunashauri kifungi hiki kifanyiwe marekebisho madogo kwa kuongeza wadau wa Afya na muda wa mapitio ya vitita vya mafao na kisomeke “Waziri, baada ya kushauriwa na Mamlaka na Wadau wa Afya atafanya mapitio ya kitita cha mafao ya msingi katika kipindi cha kila miaka 3 na vipindi vingine kwa kadiri itakavyohitajika”. 

 Maoni haya yanatokana na kifungu Na.28 cha Mswada huu kinachozitaka skimu kufanya tathmini ya uhai na uendelevu kila baada ya miaka 3 au wakati wowote … 18 (2) Uanachama (Uk.13) Kifungu hiki kinahitaji kufanyiwa marekebisho kidogo kwa kuwa kinakinzana na kifungu cha 8,9 na 10 vya Mswada huu ambavyo vimeweka masharti ya uanachama kwa kila skimu pendekezwa. 

Hivyo kifungu hiki tunapendekeza kisomeke; “Mtu kutoka sekta rasmi binafsi au sekta isiyo rasmi atajiunga na skimu ya bima ya afya kama inayopendekezwa na kifungu cha 9 na 10 cha sheria hii”.

 22 (3) Utambuzi na upatikanaji wa huduma kwa watu wasio na uwezo (Uk.14) Tunashauri kifungu hiki kifanyiwe marekebisho na kitambue mambo yafuatayo; Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha kwa kushrikiana na Waziri wa Afya kwa pamoja wataanzisha mfuko maalumu (Health Equity Fund) utakao toa huduma ya bima ya afya kwa watu wasio na uwezo nchini Vyanzo vya mapato kwa ajili ya mfuko huu vitakuwa asilimia 50% ya bidhaa zinazo sababisha madhara mbali mbali kiafya kama vile bidhaa za tumbaku, bidhaa za vileo, bidhaa ya vinywaji baridi. 

Kadhalika mapato ya ziada yatatozwa katika kodi za maliasili bila kuathiri viwango vya kodi mbali mbali ambazo tayari Serikali inachukua toka katika vyanzo hivi. 23 (1) Uwekaji wa amana (Uk.14) Tunapendekeza kifungu hiki kifanyiwe marekebisho kwa kuwa amana itakayowekwa Benki kama masharti ya usajili ni mitaji ya kampuni. Kadhalika sheria haijaweka bayana matumizi ya amana hii kama kampuni inayotoa huduma za bima itafilisika. 

 Tunashauri sheria iweke masharti ya kipindi cha muda ambao amana hii itatumika kutoa huduma kwa wanachama kama kampuni ya bima itafilisika.

 25 (3) Ukomo wa Uanachama (Uk.15) Kifungu hiki kinatoa haki zaidi kwa mwanachama anayefanyakazi katika sekta rasmi ya umma na wategemezi wake kwakuwa anapokuwa amepoteza maisha wategemezi wake wanaendelea kupata huduma za Afya lakini kwa wale wa sekta binafsi rasmi hawana fao hili. 

 Kifungu hiki tunashauri kirekebishwe kwa kuwa kinaondoa usawa kwa wanachama na wategemezi walio katika sekta rasmi binafsi au sekta zisizo rasmi wanaochangia kwa kipindi cha muda mrefu katika mifuko ya bima za Afya.

 Tunapendekeza sheria iweke masharti kwa wanachama wa sekta binafsi rasmi na zile zisizo rasmi kuwa na kiwango cha uchangiaji na idadi ya michango ambayo itawawezesha wategemezi wao kuendelea kunufaika na bima ya afya hata pale watakapo kuwa wamepoteza maisha.

 29 Uwekezaji wa skimu ya Bima ya Afya (Uk.16) Tunapendekeza pamoja na vifungu vidogo vya kifungu hiki, kuongezwe kifungu kinacho weka masharti kwa skimu kutokuwekeza katika eneo ambalo sio la afya na kutojihusisha na utoaji wa mikopo kama taasisi za kifedha. 

 30 Gharama za usimamizi na uendeshaji Tunapendekeza kifungu hiki kifanyiwe marekebisho na kiweke masharti ya viwango vya juu vya uendeshaji wa skimu na Mamlaka ya usimamizi iwe na jukumu la kupitia utekelezaji wa sharti hili na kuishauri Wizara juu ya mabadiliko ya viwango hivi katika sheria. 

 32 Zuio la kupata baadhi ya huduma pasipokuwa na bima ya Afya (Uk.16) Tunapendekeza kifungu hiki kifanyiwe marekebisho na kuhakikisha kisizuie haki za msingi za wananchi. 

Hivyo kunaweza kubakizwa baadhi ya zuio. Aidha zuio liwekwe kwa kuzingatia mahusiano ya upatikanaji wa huduma aina fulani na athari za kiafya ambapo inapelekea kuongezeka kwa gharama za afya. 

Mfano tunatambua watu wengi wanapata ajali za vyombo vya moto na hupaswa kutumia bima ya afya, hivyo huduma zinazoweza kuwekewa zuio ni kama leseni ya udereva na bima ya vyombo vya moto. 

 Pia tunashauri ili kuhamasisha wanachi kujiunga na bima, kadi za uanachama wa skimu zipewe hadhi ya vitambulisho muhimu vya kitaifa kama leseni ya udereva na kitambulisho cha NIDA ili kuhamasisha wanachi wengi kujiunga na skimu za bima ya Afya 

33 Mamlaka ya kutunga kanuni (Uk.17) Pamoja na majukumu mengine, tunapendekeza kama mapendekezo ya uanzishaji wa kamisheni ya kufanya tathmini ya gharama za Afya na yale ya mfuko wa kutoa huduma za bima ya afya kwa wale wasio na uwezo yatachukuliwa basi moja kati ya majukumu ya Waziri yatakuwa kutengeneza kanuni zitakazo ainisha;

 Uratibu wa kazi za Kamisheni ya tathmini ya gharama za huduma za Afya nchini utaratibu na uendeshaji wa mfuko wa kusaidia watu wasio na uwezo wa kujiunga na bima ya Afya (Health Equity Fund).

 39 (1) Kufutwa kwa sheria na masharti yanayoendelea Sura ya 409 (Uk.19) Taasisi ya Mkapa inapendeza muda wa kuhuisha mfuko skimu ya Bima ya Afya ya Jamii ipewe kipindi cha mwaka mmoja na nusu kwa hatua za awali na ndipo uhuishaji wa viwango nao ufuate.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana