Na William Shechambo
Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), ni chama cha kisiasa kinachoamini katika kuiongoza jamii bila ya uwepo wa matabaka ya wenye navyo na wasio navyo.
Tangu kilipoanzishwa mwaka 1921 na mwasisi wa taifa la China, Mao Zedong, chama hicho kinatajwa kuwa moja ya vyama vya siasa makini zaidi duniani.
Mwaka huu, 2022 kuanzia Oktoba 16, CPC kikiongozwa na Katibu Mkuu wake ambaye pia ni Rais wa China, Xi Jinping, kinafanya mkutano wake mkuu wa 20, mjini Beijing.
Akifungua mkutano huo, unaohudhuriwa na wajumbe 2,300 Rais Xi amezungumzia masuala yasiyopungua matano kuelekea miaka 100 mingine ya taifa hilo kubwa duniani.
Mosi anasema kuanzia sasa jukumu kuu la CPC ni kuongoza wananchi wa makabila mbalimbali nchini China, ili kujenga nchi ya kisasa ya kijamaa katika pande zote.
Pili anasema lazima chama hicho kitimize lengo la pili walilojipangia kutekeleza ndani ya miaka mia moja, ili kusukuma mbele ustawi wa taifa la China kwa njia ya kichina.
Tatu, Rais huyo Xi anasema, China inafuata sera za kidiplomasia ambazo ni huria, za kujiamulia masuala yake wenyewe kwa njia ya amani, utamaduni unaotakiwa kuendelezwa.
Anafafanua kuwa, siku zote China inaamua msimamo na sera zake kufuatia hali halisi, kulinda kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa na haki duniani.
Nne, Rais huyo anasema taifa hilo linapinga kwa nguvu, aina yoyote ya ubabe na siasa ya mabavu, pia inapinga wazo la vita baridi na vitendo vya kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine. “China haitafanya ubabe, wala haitavamia nchi nyingine daima,” anasisitiza Rais Xi.
Tano, Rais huyo anasema, anatamani kuendelea kuona China ambayo imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa nchi na maeneo zaidi ya 140, na kushika nafasi ya kwanza duniani kwa thamani ya biashara ya bidhaa.
Pia Rais Xi anasema, China inashika nafasi ya kwanza katika uwekezaji wa ndani na nje na imeendeleza sera ya kufungua mlango kwa wote kwa mapana na kina bila vikwazo.
Anasema katika hotuba hiyo kuwa, China itasimamia kwa uaminifu uanzishwaji na utekelezaji wa hatua madhubuti na tulivu katika kudhibiti utoaji wa hewa chafu na kutimiza usawa wa utoaji na ufyonzaji wa hewa hiyo.
Pia anasema, China itashiriki kwenye usimamizi wa kimataifa wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa gharama yoyote ile kwa manufaa ya dunia nzima.
Maelekezo hayo ya Rais Xi, yanapokelewa katika mkutano huo, ambao pia una wajibu wa kusikiliza na kuthibitisha taarifa ya Kamati Kuu ya 19 ya CPC, na ile ya Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Kamati Kuu hiyo.
Sambamba na hilo, mkutano huo unaotamatika Oktoba 22, mwaka huu, utathibitisha na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CPC na kuchagua na kuunda awamu mpya ya Kamati Kuu ya Chama na Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Kamati Kuu hiyo.
MAONI YA MCHAMBUZI
Akizungumzia mkutano huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa China nchini Nigeria, Charles Onunaiju, anasema mkutano mkuu wa 20 wa CPC umebeba matarajio ya dunia.
“Mkutano mkuu wa 20 wa CPC utakaofunguliwa rasmi Oktoba 16, mjini Beijing si kama tu ni jambo kubwa la China, bali pia utatoa athari za kina kwa dunia nzima,” anasema.
Anasema, mkutano huo ambao ni mwanzo mpya, dunia inaitarajia China kutimiza maendeleo zaidi na kutoa mchango mkubwa katika jumuiya ya kimataifa.
Alipozungumza katika jukwaa la warsha ya mtandaoni kwa wanahabari wa Afrika, kuhusu ushirikiano na uelewa wa China, Onunaiju anasema ameshuhudia mwenyewe maendeleo na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika muongo uliopita tangu Mkutano Mkuu wa 18 wa CPC ufanyike.
Mkurugenzi huyo anasema, kila alipokwenda China alijionea mabadiliko ya kushangaza, hasa wakati alipotembelea mikoa ya Shaanxi, Anhui, Tibet, Sichuan na Zhejiang, alishuhudia maendeleo makubwa kwenye maeneo ya vijijini, ambako wakulima wameondokana na umaskini na kuhamia katika nyumba mpya zenye mazingira bora ya kuishi.
Anasema anaona chama cha kikomunisti cha China kamwe hakijabweteka na mafanikio kiliyoyapata, na siku zote kimekuwa kikiendeleza jitihada zake kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
“Dunia inatarajia kuwa mkutano mkuu wa 20 wa CPC utachochea zaidi msukumo wa ndani wa China wa kutimiza maendeleo,” anasema.
Kadhalika anasema, anatarajia mkutano huo utaendelea kutoa ishara chanya katika kusukuma mbele maendeleo ya pamoja ya dunia nzima.
“Mathalan katika miaka kumi iliyopita tangu Mkutano Mkuu wa 18 wa CPC ulipofanyika, China imetoa misaada mbalimbali halisi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Afrika,” anasema.
Mtafiti huyo anatolea mfano ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ambao umeligusa karibia bara zima la Afrika, kwa kuweka msukumo kwenye ushirikiano wa kunufaishana kati ya Afrika na China.
Anasema mwitikio huo ambao haujawahi kutokea katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kihistoria zinazoikabili Afrika kama vile miundombinu, ni siri ya ushindi kwa urafiki wa China na Afrika.
“Miundombinu mingi ya sasa inayounganisha nchi za Afrika imejengwa chini ya mfumo wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na kutoa mchango mkubwa katika kuhimiza muunganiko na mafungamano ya kikanda katika bara la Afrika,” anasema.
Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, Chama cha Kikomunisti cha China chenye historia ya miaka 101 kimeendelea kutawala nchi hiyo kwa miaka 73, kikiwa na wanachama zaidi ya milioni 96.
Mkutano Mkuu wa Wajumbe Wote na Kamati Kuu ya Chama inayochaguliwa kwenye mkutano huo, ni mamlaka za juu zaidi za uongozi za CPC na Mkutano Mkuu wa wajumbe wote wa CPC unafanyika kila baada ya miaka mitano.
Post a Comment