Featured

    Featured Posts

AG DK. FELESHI: FANYENI KAZI MSISUBIRI VYEO

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amerejea mwito wake wa kuwataka Watumishi waliopo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majumu yao kwa weledi, uaminifu na uadilifu na siyo kusubiri teuzi au vyeo.

Ametoa rai hiyo leo, Alhamisi wakati wa mazungumzo yake na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt Bonifance Luhende na Naibu Wakili Mkuu  Bi. Sara Mwaipopo waliofika Ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Menejimenti, Mawakili Wakuu na Mawakili Waandamizi wote kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Dkt. Feleshi amesema, uongozi hautafutwi, uongozi unakuja kwa kufanyakazi.

“Niwapongeze kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwenu na Mhe. Rais kushika nafasi hizo za uongozi. Uongozi hautafutwi, tekeleza majukumu yako, jukumu ulilonalo mkononi ndilo lako, timiza wajibu wako na mengine yatafuata”, amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria kuu wa Serikali, amesisitiza haja na umuhimu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa na ushirikiano wakaribu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo kimsingi Ofisi hiyo inatekeleza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali .

Akielezea zaidi kuhuhusu haja na umuhimu wa Ofisi hizo mbili wa kufanyakazi kwa karibu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kuwa taratibu kadhaa zimeshawekwa zikiwamo za kuwa na maafisa dawati wanaoratibu mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa kwa haraka na kwa wakati baina ya Ofisi hizo mbili.

Naye Wakili Mkuu Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance Luhende amemhakikishia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba, yeye binafsi, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi yote wanalichukulia suala la uhusiano na Ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni jambo la kipaumbele.

Dkt. Lunhede amesema, Ofisi hizo mbili ni kiungo muhimu katika kuisadia Serikali kufikia malengo yake yakiwamo ya kuwaletea wananchi maendeleo, lakini pia ni Ofisi ambazo mambo mengi na mazito yanapita kwenye Ofisi hizo, mambo ambayo wakati mwingine yanahitaji ushauri na maamuzi ya haraka hivyo ushirikiano na mawasiliano kati yake ni jambo ambalo halikwepeki.

“Ofisi zetu hizi zina mambo mazito yanayopita mikononi mwetu, mambo yanayohitaji wakati mwingine kutoa ushauri na maamuzi ya haraka kwa Serikali ili mambo yaweze kwenda, kwa hiyo kwetu sisi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jambo la ushirikiano na Ofisi yako, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunalipa kipaumbele”, amesisitiza Wakili Mkuu wa Serikali.

Amebainisha kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo ni muhimu kwa Ofisi hizo kuwa na mwelekeo na maono ya pamoja ili kuisaidia Serikali.

“Tunatekeleza majukumu yetu kwa niaba yako Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunapaswa kuwa na maono na uelewa wa pamoja, tunapaswa kucheza kama timu moja, hakuna mchezaji anayeweza kushinda bila ya ushiriki wa wachezaji wengne,  lengo letu si kushindana bali kuisaidia serikali ishinde” Akasema Wakili Mkuuwa Serikali.

Aidha katika mazungumzo hayo, Ofisi hizo mbili pia zimekubaliana kuwatumia Mawakili wa Serikali waliomo katika kazi Data ya Mawakili wa Serikali inayoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pale watakapohitajika kuisaidia serikali kwa mijibu wa taaluma zao,  uwezo na uzoefu wao katika masuala mbalimbali.

Oktoba 10, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwateua Dkt. Boniface Christopher Luhende kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na alimteua pia Bi. Sara Duncan Mwaipopo kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali. 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akisisitiza jambo wakati Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface  Luhende  na  Naibu  Wakili  Mkuu wa Serikali Bi. Sara Mwaipopo walipomtembelea Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma, na kisha kuwa na  mazungumzo ya pamoja na Menejimenti  ya Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawakili  Wakuu wa Serikali na  Mawakili Waandamizi wa Serikali, leo. 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer  Feleshi akimkaribisha Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Luhende pamoja na Naibu  Wake Bi. Sara Mwaipopo wakati walipomtembelea Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na kisha kuwa na mazungumzo na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, leo.

Wakili  Mkuu wa Serikali Dkt.  Boniface  Luhende akipokea shada la maua kutoka Bi. Consolata Magohe mara baada ya kuwasili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwa ameambanata na  Naibu Wakili  Mkuu Bi. Sara Mwaipopo ambaye pia alikabidhiwa shada la maura ikiwa ni sehemu ya kuwakaribisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, leo. (Picha zote na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serkali).
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana