Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mohamed Ali Mohammed (Kawaida) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Uchaguzi uliofanywa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo, katika eneo la Mtumba, kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, jana.
Akitangaza matokeo hayo aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson alimtangaza Kawaida kuibuka na ushindi katika Uchaguzi huo kwa kupata kura 523 akiwashinda Farid Mohammed Haji aliyepata kura 25, Kassim Haji Kassu kura 2 na Abdallah Ibrahim Natepe kura moja.
Kufuatia hatua hiyo, Kawaida ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Kusini Unguja anachukua nafasi ya Kheri James ambaye mwaka jana (Juni 2021) Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
Mara baada ya kumtangaza wajumbe walilipuka kwa kuimba "Kawaida Kawaida", huku wakimbeba kwenda meza kuu.
Uchaguzi wa UVCCM umefuatia ule wa Jumuiya ya Wazazi, uliofanyika majuzi, jijini Dodoma ambapo Fadhil Muganya alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.
Katika kukamilisha Uchaguzi katika Jumuiya za CCM ngazi ya Taifa, leo ni zamu ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao watachuana mbele ya Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kuwa mgeni Mkuu katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Jumuia, Jijini Dodoma.
Post a Comment