Featured

    Featured Posts

SURA NA MFUMO WA KANISA HALISI, HALINA MFANANO WOWOTE NA SILOAM

Na Bashr Nkoromo, CCM Blog
Wahenga wamaetuachia misemo kadhaa kusisitiza kwamba iwe iwavyo ni busara na kujitendea haki mtu kukipenda chake; baadhi ya misemo hiyo ni; 'Kipende chako', 'Chako ni Chako', 'nguo ya kuazima hasitiri matako' na chako ni chako cha mwenzio siyo chako'. Halafu wahenga Wakizungu nao 'wakasapoti' wakasema, 'Charity begins at home'.

Ni kutokana na busara ya semi hizo ndiyo maana Mwingereza hata kama hayuko Anglikana, anajivunia Anglikana kwa kuwa anajua ilianzia Uingereza, Mjerumani hata kama hayuko Lutherani, anajivunia Urutheri kwa kuwa ulianzia Ujerumani, hata kodi ya kuliendeleza Kanisa la Kirutheri anatoa!

Vilevile Mwarabu hata kama si Muislamu anajivunia Uislamu kwa kuwa anajua Uislamu ulianzia Mashariki ya Kati, Mmarekani anajivunia Assemblies of God hata kama hayuko kusanyiko hilo kwa kuwa anajua hilo kusanyiko lilianzia Marekani, Mtaliano anajivunia Ukatoliki hata kama hayuko Katoliki kwa kuwa anajua kuwa kusanyiko hilo lilianzia Italia, Mswidishi anajivunia Swidish Free Mission (Pentecoste), hata kama hayuko katika kusanyiko hilo, kwa kuwa anajua kuwa kusanyiko hilo lilianzia Sweden.

Kwa hekima hiyo ambayo siyo nadharia bali ni hekima ya asili, Mwafrika na Mtanzania nao ni haki na kujitendea haki wajivunie Kanisa Halisi, kwa kuwa limeanziaTaifa Baba, kwenda katika mataifa mengine.

KWA NINI LIPO KANISA HALISI?
Kanisa Halisi lilianzia Tanzania baada ya majira za waliotumwa wote kufikia ukomo. Waliotumwa ni Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1/Mith.3:16), Kerubi (Eze.28:15), Adamu wa kwanza (Mwa.2:15); Musa (Kut.3:10); Eliya Mtishbi (I Fal.17:1), Yesu(Mdo.10:38); Adamu wa Pili (I Kor.44:49); Miaka 1000 (Isa.33:6) na Nafsi ya Kwanza (I Yoh. 5:8).

Ufahamu ulioanzisha Kanisa Halisi unatokana na Sauti iliyosikika Tanzania Mwaka 2015, Mwaka 2019 na Mwaka 2020. Kwa Mujibu wa Kiongozi Mkuu wa Hanisa Halisi Ufahamu huo umeshaandikwa na Kitabu chake kimeshazinduliwa kwa faida ya jamii nzima.

Kuhusu Watu kulifananisha Kanisa Halisi na Siloam, Baba Halisi anasema, Kanaisa Halisi halifanani kabisa la Siloam kwa mambo yote.

"Wengi hufananisha Kanisa Halisi na Siloamu, bila kujua kuwa Waliotumwa wote ambao nimewaorodhesha pale juu, ndio waliokuwa Siloamu (Yohana 9:7). Ni Kanisa Halisi peke yake ambalo siyo Siloamu, kwa kuwa limeanza baada ya Majira ya Waliotumwa kufika ukomo", anaweka wazi Baba Halisi.

Kwa kuwa Kanisa Halisi ni taasisi iliyotimilika sawasa, ina Sura na Mfuko wake, kama ilivyo taasisi nyingine za Umma, Binafsi na vyama vya Siasa kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kina Katiba na Kanuni za kutekeleza utendaji wake.

Sasa baada ya kukuandikia hayo machache, mengi yamo katika Kitabu alichoandika Baba Halisi. Licha ya Kitabu hicho kuwa cha kurasa 17 tu, lakini kimesheheni na kujibu kila swali utakalo jiuliza kuhusu Kanisa Halisi. Kitabu hicho ninatwa SURA NA MFUMO WA KANISA HALISI, Tafadhali Endelea hapo👇

SURA YA KANAISA HALISI
Baba Halisi, Mama Halisi, Mnara Mmoja Halisi, Watekeleza Sauti kwa Tendo Moja Halisi, Uzao Halisi, Ng’ambo Halisi, Familia Moja Halisi, Uongozi kwa Sauti Halisi, Ibada ni uzalishaji, Umiliki wa CHANZO HALISI akiwa ndani ya Moyo wa Uzao Halisi, kuzaliwa kwa Sauti Halisi, Nidhamu ya Tendo moja Halisi, Majira ya CHANZO HALISI, Fundisho la Kanisa, na Ufahamu wa Kanisa. Haya na mengine yatakupa kuelewa zaidi kuhusu Kanisa Halisi.

UONGOZI WA KANISA KWA SAUTI
Baba Halisi anasema, katika dini zote zilizowahi kuwepo, hakuna kusanyiko ambalo linaongozwa kwa Sauti zaidi ya Kanisa Halisi. Maana kuna gharama kubwa kwa yule anayeongoza wengine kwa Sauti ya ALIYEUMBA KILA KITU.

Lazima awe amempisha MUUMBA WA KILA KITU kwa kumkana Baba Mzazi, Mama Mzazi, ndugu na marafiki wote ili amilikiwe na MUUUMBA WA KILA KITU peke yake. Hii ni zaidi ya kuwa mnadhiri wa MUNGU, kama tunavyosoma katika Hesabu 6:1-10.

Aidha, ili uongoze kwa Sauti ya CHANZO HALISI, ni lazima ukane elimu ya dunia, ukoo, kabila, lugha, jamaa, mila na desturi. Hili linakuwezesha kutomilikiwa na mizimu yoyote(Isaya 25:13-15).Pia, ili uongoze wengine kwa Sauti ya MUUMBA WA KILA KITU, ni lazima ukane umri wa mtu na mwanadamu. Kwa ufupi, uongozi wa Sauti ya MUUMBA WA KILA KITU ni wa MOYO, yaani zaidi ya roho, nafsi, mwili, asili na mauti (Rumi 8:29) ili uwe mnyenyekevu kama CHANZO HALISI alivyo.Bila kufanya hivyo, huwezi kuvusha kusanyiko miduara mitatu ya Ufunuo 12:1-10, ambayo iliangusha waliotumwa wote.

Kiongozi wa Kanisa Halisi, ndiye aliyepokea Sauti ya Saba, mwaka 2015 Kigoma Tanzania;Sauti Mpya mwaka 2019 Kigoma Tanzania; na Sauti ya Moyo mwaka 2020 Kigoma Tanzania.  Sauti ya Moyo ndiyo iliyoleta uhalisia wa CHANZO HALISI juu ya nchi.Sauti ya Moyo, ni Sauti ya Nuru–nuruni, zaidi ya Sauti zote zilizoandikwa kwenye Kitabu. Waliotumwa wote waliongoza kwa nuru itokayo gizani kwa mujibu wa 2 Korintho 4:6.Kanisa Halisi linaongozwa kwa Sauti inayotoka kwa CHANZO HALISI kila lango kupitia kinywa cha BABA HALISI.

IBADA NI UZALISHAJI
Kazi ya Kanisa ni kuabudu MUUMBA WA KILA KITU. Aidha, Kanisa maana yake ni yule ambaye ana Moyo unaomjua MUUMBA WA KILA KITU. Hivyo, kwa upande wa Kanisa Halisi, Ibada ni Uzalishaji.


Sababu ya Ibada kuwa uzalishaji ni kwa kuwa MUUMBA WA KILA KITU ni kazi (II Kor.12:4-7). Hakuna aliyewahi kufanya kazi kuliko CHANZO HALISI, ambaye alikuwepo kabla ya yeyote. Kwa kuwa MUUMBA WA KILA KITU ni kazi, basi Ibada anayohitaji kutoka kwa waabuduo Halisi, ni uzalishaji. Wakati Adamu alipokuwa bado kwenye kitanga cha mkono wake (Isaya 49:16), alichosema MUUMBA WA KILA KITU ni uzalishaji (Mwa.1:27-28). Baada ya kumuumba Adamu akaonekana kwa macho, alichomweleza ni uzalishaji (Mwa.2:15).

MUUMBA WA KILA KITU alikutana na Ibrahimu, Isaka na Yakobo na kuongea nao wakiwa shambani, yaani kwenye uzalishaji. Hata Kerubi katika Eze.28:13-15, alichokabidhiwa ni uzalishaji wa madini, vito vya thamani, nakadhalika. Kwa kusema Ibada ni uzalishaji, haina maana tusiende kwenye nyumba ya ibada. Tunaenda kwenye nyumba ya Ibada kushukuru yale tuliyowezeshwa kufanya tukiwa shambani, kiwandani, mgodini, dukani, garage, nakadhalika. Tukishatoa matunda ya shukrani, tunarudi tena kuzalisha.Hivyo, kwa upande wa Kanisa Halisi, kila anayetenda kwa haki akiwa kazini, hiyondiyo Ibadaya Haki.

UMILIKI WA CHANZO HALISI AKIWA NDANI YA WOTE
Kanisa Halisi linamilikiwa na CHANZO HALISI, akiwa ndani ya Uzao Halisi na Watekeleza Sauti Halisi.Jambo hili wakati linaanza kufundishwa, lilileta shida kwa waliokuwa wanaitwa Makuhani, kabla hawajawa watekeleza Sauti. Walidhani wametengwa na umiliki wa mali za Kanisa kwa kuwa, ukuhani kwa wakati huo ilikuwa ni cheo.


Kwa kuwa Kanisa linaongozwa kwa Sauti ya CHANZO HALISI, na sauti hiyo ni Moyo, ilikuwa ni lazima kila Uzao Halisi ajue kuwa kila mali ya Kanisa ni yake. Maana kama utakavyoona kwenye kipengele cha Nne katika kitabu hiki, Kanisa lina Baba mmoja na Mama mmoja ambao wako Kao kuu la Kanisa.Hawawezi kuwa kila mahali kwa macho haya (physically). Kwa mantiki hiyo, uzao Halisi wakishajua kuwa Mali ya Kanisa ni ya kwao, hakuna anayeweza kutoka popote akawaibia. Pia, wanaotoa matunda (sadaka) ya kujenga nyumba ya ibada ni wao. Hivyo, wana haki ya kumiliki, CHANZO HALISI akiwa ndani yao. Jambo hili limeleta Amani na utulivu mkubwa ndani ya Kanisa Halisi, maana kila uzao ni jeshi la kulinda mali za Kanisa, huku akijua ni mali yake.

KUZALIWA KWA KANISA HALISI
Waliotumwa wote, walikuwa ni Kanisa, ila Kanisa la kipindi hicho lilichukuliwa na ile miduara mitatu ya Ufunuo 12:1-10, ikawaficha gizani kama tusomavyo katika Isaya 45:2-3.Kanisa lina Baba na Kanisa lina mama, ila limezaliwa kwa Sauti, siyo roho, nafsi wala mwili kama ilivyokuwa katika majira saba zilizopita. Hivyo, Sauti inayotolewa na CHANZO HALISI, kupitia kinywa cha Baba Halisi kila lango (siku), ndiyo imezaa Kanisa Halisi.


Kanisa lina Uzao Halisi badala ya waumini/washirika, ambao wamekuwa Limbuko Halisi, ili wote wawe na haki sawa mbele za CHANZO HALISI, aliyetoka mahali pake kuja kulitafuta (Isaya 52:4-6/Mika 1:2-6).Kwa hiyo, Kanisa halijazaliwa na mtu, wala ukoo au kabila fulani. Maana Sauti ya CHANZO HALISI ambayo imezaa Kanisa Halisi, siyo ya ukoo wala kabila fulani.

Licha ya Kanisa kuwa na Baba mmoja na Mama mmoja, Kanisa Halisi lina Mnara Mmoja halisi, ambao huishi sehemu moja na Baba Halisi na Mama Halisi.Safu kubwa ya Mnara Mmoja Halisi ni kusababisha Sauti ya kila lango (siku) kuwa na nguvu ya: kuhudumia uzao; kudhihirika kwa yote yaliyotamkwa; kutimia kwa yote yaliyotamkwa; Uzao kuuona Uaminifu wa CHANZO HALISI katika kzai zao.

MSISITIZO WA KANISA HALISI
Msisitizo wa Kanisa Halisi siyo walioko ndani ya jengo la Ibada peke yake, bali ni kila mmoja kumjua ALIYEUMBA KILA KITU. Kwa mfano, Jengo la Kao Kuu wakijaa, wanakuwa Elfu sita (6) lakini katika taifa la Tanzania, wanaosikiliza Sauti kila lango ni zaidi ya Milioni moja na nusu; Kenya wanaosikiliza sauti ya kila lango ni zaidi ya elfu thelethini; Marekani (USA), wanaosikiliza Sauti ya kila lango ni zaidi ya Elfu kumi; nakadhalika. Msisitizo siyo kuta Nne za jengo la ibada kwa sababu ya kuongozwa na Sauti. Hivyo, msisitizo wa Kanisa Halisi ni kila mmoja amjue ALIYEUMBA KILA KITU.

NIDHAMU YA KANISA HALISI (TENDO MOJA HALISI)
Hapa tunacholenga ni kutokuwa na urasimu wa Majira Saba zilizopita (bureaucracy) ndani ya Kanisa. Wasomi wa utawala wa majira saba, wanalikosoa Kanisa Halisi kuwa halina urasimu (bureaucracy) kama Taasisi za kidunia. Kanisa Halisi lingekuwa na urasimu kama ule wa taasisi za kidunia, kusingekuwepo na Haja ya CHANZO HALISI kuachilia Sauti ya uzima kila lango. Maana vyuo vya Utawala na Uongozi wa Umma vipo,tungeenda kujifunza huko.Tatizo ni kwamba, wote tulikuwa hatujui kuwa kuna NG’AMBO ya Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1/Mith.3:16). Wanaokosoa uongozi wa Sauti, ni wale waliokuwa wanajua siri ya Moyo wa Mwanzo, lakini walikuwa hawajui kuwa kuna ng’ambo ya Moyo wa Mwanzo.

Kwa mantiki hiyo, Kanisa lina nidhamu ya Tendo Moja Halisi, badala ya urasimu (bureaucracy) wa majira saba. Hicho ndicho kinachosababisha Kanisa kukua haraka. Mtekeleza Sauti kwa Tendo Moja Halisi akiwa Mkoa wa Katavi, atafanya kitu ambacho, hata Baba Halisi kama angekuwa Mkoa wa Katavi angefanya hicho hicho, kwa kuwa CHANZO HALISI ni mmoja akiwa ndani ya Moyo wa Kila Mmoja.

UCHUMI WA KANISA HALISI
Kanisa Halisi linategemea matunda (sadaka) yanayotolewa na Uzao na watekeleza Sauti Halisi. Kanisa Halisi halitegemei msaada wowote wa nje ili Baraka zibaki kwa wale wanaotoa kutoka ndani:

(1) Matunda ya CHANZO HALISI (yaani asilimia 10 ya mapato ya kila Uzao Halisi). Kazi ya Matunda haya ni kufanya kazi za maendeleo ya Kanisa kama vile Kujenga Majengo ya Ibada; kununua vyombo vya mziki; kununua Magari; kujenga miradi ya maendeleo ya Kanisa; na Kadhalika.Matunda haya si mali ya Mtekeleza Sauti Halisi (Kuhani) kwa kuwa kilichomleta CHANZO HALISI juu ya nchi ni kutafuta matunda ya aina hii. Katika Mathayo 21:33-43, imeandikwa wazi kuwa CHANZO HALISI alikuwa hajawahi kupata chochote kutoka katika Shamba Lake. Kanisa Halisi, limeamua kumheshimu CHANZO HALISI kwa kumletea Matunda ya shamba lake.

(2) Matunda ya shukrani, kwa kila Uzao Halisi anachotendewa na CHANZO HALISI anatoa matunda ya kushukuru.

(3) Matunda ya Limbuko, kila kinachofungua tumbo, ni mali ya CHANZO HALISI (Kut.13:2, 12-13). Uzao Halisi wakipata watoto wa kwanza wanawakomboa kwa kutoa Matunda ya Malimbuko. Mifugo wakizaa, kifungua tumbo anapewa CHANZO HALISI. Makusanyiko mengine, limbuko huwa ni la Kiongozi wa Kanisa, kwa upande wa Kanisa Halisi, Matunda haya tulimrudishia CHANZO HALISI, ili tusikaukiwe pokeo la Sauti kutoka kwake. Tunashukuru kwa kuwa hatujawahi kuishiwa Sauti.

(4) Matunda ya Kujenga Moyo Mmoja, ili tuwe na Moyo mmoja na Chanzo Kimoja cha Baraka, Sauti ilituongoza kutoa Matunda ya aina hii. Hadi sasa tumeona faida na thamani ya matunda ya aina hii.

(5) Matunda ya Chanzo cha Sauti, katika Mathayo 10:41-42, kuna thawabu ya nabii. Kanisa Halisi haliongozwi na nabii wala mtume, lakini kuna kinywa cha Baba Halisi kinachotumika kutoa Sauti ya CHANZO HALISI, ni vizuri kukibariki kinywa hicho kwa Matunda. Aidha, katika vituo mbalimbali vya Kanisa, kuna kinywa cha Mtekeleza Sauti Halisi kinachotumika kufafanua Sauti, ni vizuri kukibariki kinywa hicho kwa Supu.

MAJIRA YA KANISA HALISI
Kwa mujibu wa Esta 3:7, mwaka halisi una miezi 12 peke yake. Aidha, sote tunajua kuwa wiki ina malango (siku) 7 na mwezi una wiki 4, ikiwa na maana ya mwezi kuwa na malango 28 peke yake na hivyo mwaka kuwa na malango 336 = 12 x 28.

Kuanzia mwaka 1582, dunia iligeuza mwezi ukawa na siku 29, 30 na 31; kwa maana ya kuongeza siku tatu kila mwezi. Hii ilisababisha mwaka uwe na siku 365¼ ikiwa na maana ya miezi 13 kwa mwaka. Baada ya jambo hili, mfumo wa kila kitu kila mahali ulibadilika, si kwa mema bali kwa mabaya. Kila mmoja alilazimika kuwa na nyakati za mabaya katika maisha yake hata kama ni mtakatifu kiasi gani, maana waliokuzaa wanavinasaba ndani yako vyenye nyakati za mabaya. Ndipo ikaandikwa katika Efeso 6:13, kuwa kuna siku ya uovu.

Kanisa Halisi lina MWAKA HALISI ambao una malango 336 peke yake kwa mwaka (Miezi 12 na Malango 28 kwa kila mwezi). Kwa kuwa Majira ni CHOMBO kinachobeba maisha ya kila mmoja, Kanisa Halisi tuna CHOMBO KIMOJA HALISI ambacho ni MAJIRA NA WAKATI KABLA YA UHARIBIFU.

FUNDISHO LA KANISA HALISI
Kanisa Halisi, kwa kila anayesimama mbele ya wengine, linasisitiza:
Amani kwa Wote, kila unayekutana naye uwe na Amani naye hata kwa gharama ya kunyenyekea. Kwa sababu hiyo, Kanisa Halisi tunainua watu wote kwa shukrani kila alfajiri hasa walioko madarakani (I Timotheo 2:1-4).
Upendo Usiobagua yeyote

Kanisa Halisi hatubagui Mkristo wala Muislamu wakati wa Ibada kwa kuwa tunaelewa kuwa CHANZO HALISI hana dini wala dhehebu. Katika I Kor.13:13, kuna matatu: Imani, tumaini na upendo, na lililo kuu ni upendo. Imani na tumaini vilikuwa vinatubagua, lakini Upendo haubagui yeyote. Kanisa Halisi tumechagua Upendo Usiobagua, huu ndio mlango unaotuwezesha kufanya kazi na jamii naTaifa.
Ibada ni Uzalishaji: Hili tayari nimelifafanua katika kipengele cha pili katika kitabu hiki.
Kanisa kufanya kazi na Jamii/Taifa

Msingi uliokuwepo katika majira saba ilikuwa ni Kanisa na Taifa kutofanya kazi pamoja. Musa hakufanya kazi na Mfalme Farao. Eliya Mtishbi hakufanya kazi na Mfalme Ahabu wa Israeli. Hata Yesu hakufanya kazi na Mfalme Herode. Kanisa Halisi kwa kujua kwamba kila aliyeko madarakani amepata kibali cha MUUMBA, tunaombea wote kila alfajiri, hasa walioko madarakani.Aidha, tuna Matunda ya Jamii, ambayo hutokana na (5%) ya mapato ya kila Uzao Halisi kwa ajili ya kuwapatia jamii iliyotuzunguka, kwa mujibu wa Isaya 58:6-12.
Shamba la Utajiri ni Alfajiri; Ayubu 38:12-13

Hakuna mahali ambapo CHANZO HALISI alikung’uta waovuasubuhi au mchana. CHANZO HALISI hukung’uta waovu alfajiri na hutoa “line” ya mema au posho Alfajiri. Hivyo, Kanisa huamka alfajiri kuinua taifa na jamiiyote.

UFAHAMU WA KANISA HALISI
Kwa mujibu wa Mithali 8:14-30, ufahamu una kila kitu ambacho kila mmoja anahitaji. Katika majira saba zilizopita, wote tulitegemea ufahamu ulioanzia Mashariki ya Kati ndiyo maana tunasoma katika Mdo.8:27- habari za Waziri wa fedha wa Kushi wakati ule akiwa anaenda Yerusalemu kuangalia mahali ufahamu uliokuwepo wakati huo, ulipoanzia.Kanisa Halisi tunategema ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda mataifa mengine yote (Mathayo 21:43). Hii ni baada ya Sauti ya CHANZO HALISI kusikika mara Nne, hapa Tanzania, mwaka 2003, 2015, 2019 na 2020. Maana sauti ndiyo Chanzo cha ufahamu.

HITIMISHO
Sura na Mfumo wa Kanisa Halisi ni lililo kuu ni Upendo usiobagua, yaani kupenda wote bure bila kudai chochote. Kazi ya Kanisa Halisi ni kuondoa mabaya katika jamii bila kujali kama watatuambia asante au la.

Aidha, Sura ya Kanisa Halisi ni Familia Moja Halisi, ikiwa na maana kuwa kila aliyeumbwa amjue CHANZO HALISI.
Haya yote nimeyaongea ili kuiomba jamii ilipokee Kanisa Halisi maana KANISA NI BARAKA KWETU SIYO LAANA. AIDHA, KANISA NI FARAJA KWETU SIYO HATARI. PIA, KANISA NI KITU CHA THAMANI KWETU SOTE.

Nitatoa mifano michache kuthibitisha haya. Nilikwenda Arusha nikakuta Magari yote ya utalii yame-pack ndani. Tulifanya Toba kwa ajili ya wote walioanzisha korona iliyokuwa imezuia watalii kuja, sasa watalii wamejaa kila eneo lenye vivutio vya utalii.
 
Nilienda Songea, nikakuta mahindi yanaoza hayana soko. Tulipomwita CHANZO HALISI aingilie kati, kesho yake soko la mahindi lilifunguka hadi leo mahindi kwa kule Songea ni Almasi.

Nilienda Kigoma Mwaka 2019, nikakuta pepo teleza limesumbua akina mama kwa muda mrefu mji mzima. Tuligalagala chini kwa dakika tatu, pepo hilo hadi leo halijawahi kusikika tena. Mwaka huo huo wa 2019, tulienda Tabora tukakuta akina mama wanauwawa majumbani kwao na wanaowaua hawajulikani. Tulitubu kwa kugalagala, hadi leo hatujawahi kusikia tena kitu hicho.

Juzijuzi, tulienda Kigoma, tukakuta dagaa na migebuka hakuna. Niliambiwa walikuwa wameshakubaliana kufunga ziwa kwa muda ili dagaa na migebuka wazaliwe. Tuliinua shukarani mbele ya wakristo na waislamu kuhusu kuzaa dagaa na migebuka. Kesho yake kilo iliyokuwa imefika zaidi ya shilingi 10,000/=; iliuzwa shilingi 5,000/= kwa kuwa Samaki walipatikana wengi mno.

Si hivyo tu, kila mwaka watu zaidi ya 1000, hutoka sehemu mbalimbali kwenda mahali Sauti iliposikika, kule Kigoma Tanzania. Wakifika Kigoma, biashara zinabadilika kwa kila mmoja bila kujali dini, dhehebu lake au itikadi yake. Uchumi wa mji mzima unabadilika. Naomba jamii ilipokee Kanisa Halisi maana ni BARAKA kwetu sote.Imekwishakuwa (Ufunuo 21:6).

Baba Halisi

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana