Na Mwandishi Maalum, Chinangali, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer Feleshi amemhakikishi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwamba ataendelea kusimamia kwa karibu maelekezo aliyotoa tarehe 29 Septemba 2022, ambayo yalitokana na maelekezo ya awali ambayo yeye Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyatoa kwa Watendajiwa Serikali.
Maelekezo hayo pamoja na mambo mengine ni ya kuwataka Watendaji Wakuu wa Serikali kutoa kipaumbele cha kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali Septemba 29 2022 pia pamoja na mambo mengine Rais Samia aliwataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanakuwa makini kusikiliza migogoro na kuhakikisha inatatuliwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Dk. Feleshi ambaye ametoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Shera Nchini ambapo Rais Samia alikuwa mgeni rasmi amesisitiza kuwa Ofisi yake (OMMS) na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG) pia zitaendelea utekeleza maelekezo ya kusimamia kwa niaba ya Serikali matakwa ya kisheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Maadhimisho hayo yamefanyika Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi wa Mahakama, Serikali, Bunge, Mawakili, Wanafunzi na wananchi.
Mwanasheria MkuuwaSerikali aliyezungumza baada ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea ( TLS) Profesa Edward Hosea kuzungumza, alisema pamoja na kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Rais pia ataendelea kusimamia maelekezo aliyoyatoa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo Machi 30, 2022 kwa Watendaji Wakuu Serikali ya kuwataka pamoja na mambo mengine kutoa kipaumbele cha kumaliza migogoro kwanjia ya maridhiano.
Dk. Feleshi amebainisha pia kwamba, maelekezo yake hayo pia aliyapeleka kwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye naye aliwasisitiza Watendaji wa Srikali kuwa hatua ya uvunjaji wa mikataba iwe ni suluhisho la mwisho baada ya njia zote za majadiliano kushindikana na kwamba uvunjaji huo ufanyike kwa kibali cha Mwanasheria Mkuuwa Serikali.
Pamoja nakusisitiza kuwa atasimamia maelekezo ya Rais na yale mbayo yeye aliyatoa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Eliezer Feleshi alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watendaji wa Serikali kuzingatia maelekezo hayo muhimu ili kuyiishi kwa vitendo kaulimbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka 2023.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia altoa rai kwa Majaji na Mahakimu kuwa tayari kuwasilisha ofisini kwake kupitia dawati linaloshughulika na utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali kuhusu wakili yeyote wa Serikali ambaye kwa namna yoyote atathibitika kudhoofisha jitihada za Serikali na Mahakama za kutumia njia za usuluhishi katika kutatua migogoro.
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema wakati umewadia wa kuboresha tena Sheria ya Mwenendo wa Madai, Sura ya 33 ili shauri la madai lipate sifa ya kusajiliwa mahakamani endapo kuna uthibitisho kwamba limepitia hatua zote za usuluhishi na ikashindikana.
Mapema katika hafla hiyo Rais Samia ameagiza Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na kuzifanyia marekebisho sheria zenye mizunguko mingi na hivyok uchelewesha utoaji wa haki.
Naye Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Juma amepongeza mapendekezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kuzifanyia mabadiliko baadhi ya sheria zenye milolongo mirefu na kwamba marekebisho hayo yatasaia sana.
Pia Jaji Mkuu ametoa rai kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama liwe la lazima na jambo hilo limo ndani ya uwezo wake.
Kaulimbiu ya Siku ya Sheria nchini ilikuwa umuhimu wautatuzi wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau”.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu baada ya Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maadhimisho ya siku ya Sheria yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma. (Picha zote na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali)
Post a Comment