Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa komputa mpakato (Laptop) 150 kwa ajili ya mawakili wa Serikali ikiwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba mwaka jana.
Vifaa hivyo vya Tehama, vimekabidhiwa jana Jumatano Machi 22, 2023, kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Moses Mpogole Kusiluka, kwa niaba ya Rais Samia, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dodoma na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Sylvester Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Boniphace Luhende.
Akizungumza katika hafla ya hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Kusiluka amesema, ni matumaini ya Rais kuwa, vifaa hivyo vya tehama vitaboresha na kuongeza ufanisi wa Mawakili wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Tumekutana katika hafla hii fupilakini muhimu sana. Rais alitoa maelekezo tukutane ili nikukabidhi vifaa hivi vya Tehama ambayo aliridhia wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba 2022 hapa Dodoma.
Ni matarajio ya Rais kuwa vitendea kazi hivi vitatumika kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya mawakili wa Serikali hasa kwa kuzingatia umuhimu wa matumizi ya tehama katika tasnia ya sheria”, akasema Katibu Mkuu Kiongozi.
Katibu Mkuu kiongozi Kusiluka akaeleza zaidi kwa kusema “Sote tunafahamu Mhe. Rais ametoa kipaumbele katika kuboresha mifumo ya haki jinai na haki kwa ujumla, hivyo basi juhudi za Rais na serikali kupitia msaada huu ni kuona ufanisi wa mawakili wa serikali nao unaongezeka”.
Katibu Mkuu Kiongozi Kusiluka, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia Mawakili wa Serikali kadri itakavyowezekana hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imejikita katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo inahitaji wataalamu wabobevu katika kila eneo wakiwamo Mawakili wa Serikali.
“ Serikali inathamini mchango wa Mawakili wa Serikali, ni matumaini ya Rais na ya kwangu kwamba, ninyi viongozi wa Taasisi mtaendelea kusaidia na kuhamasisha wataalamu wenu kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati” akasisitiza Katibu Mkuu Kiongozi.
Akizungumza baaada ya kukabidhiwa vifaa hivyo vya Tehama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Feleshi, amesema Komputa mpakato hizo zitaleta heshima na ufanisi zaidi wa kazi kwa Mawakili wa Serikali.
“Kwa niaba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais, kwa kuridhia na kutupatia vifaa hivi vya tehama, ametuangalia kwa jicho la umama na kwa kweli ni upendo wake wa dhati” akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akasema, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika Septemba 29 mwaka jana, ambao Rais alikuwa mgeni rasmi na akazindua Chama cha Mawakili wa Serikali, alibainisha changamoto mbalimbali zikiwamo za uhaba wa vitenda kazi kwa maana ya Vifaa vya Tehama kwa mawakili wa Serikali
“Katika Mkutano ule tulielezea changamoto mbalimbali zikiwamo za miundombinu, upungufu wa watumishi, lakini pia tukaelezea hili la vitendea kazi kwa maana ya vifaa vya tehema ili kwenda sanjari na maboresho yanayoendelea katika Tasnia ya Sheria.
Hata katika majadiliano ya migogoro baina ya Serikali na Wadau wetu, vikao vingi vinafanyika kwa njia ya Tehema jambo ambalo Mawakili wetu wapo nyuma kutokana na kutokuwa na vitenda kazi vya kisasa, vifaa hivi vitaleta heshima kubwa kwa mawakili wetu wa Serikali wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao” akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali Dk. Feleshi, akasema, vifaa hivyo vya Tehama si kwamba vinahitajika kwa Mawakili wa Serikali peke yao bali hata kwa Divisheni na Vitengo wezeshi akitolewa mfano wa Kurugenzi ya Utawala na Raslimali Watu, Kurugenzi ya Mipango na Masijala.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi, tunafahamu mchakato huu umegharimu fedha na muda wa Mheshimiwa Rais na Serikali, sisi sote hapa ni wateule wa Rais na ukisha kuwa mteule wa Rais huna mambo yako, tunafuatilia na kusikiliza shughuli za Mheshimiwa Rais, niahidi kwamba tutatumia vifaa hivi ili kwa pamoja na Serikali tuweze kuleta nafuu kwa Watanzania”, akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akitoa shukrani zake kwa Mhe. Rais baada ya kupokea vifaa vya Tehama kwaajili ya matumizi ya Mawakili wa Serikali . Vifaa hivyo viliombwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika mwezi Septemba 2022 na mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungnao wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende nao walikuwepo katika hafla hiyo ya makabidhiano ya vifaa hivyo vya Tehama iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Dodoma. Vifaa hivyo vya Tehama vitaganywa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe Dkt. Moses Kusiluka (kushoto), akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe Jaji. Dkt. Eliezer Feleshi, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa wakiangalia maboksi yenye vifaa vya Tehama ( komputa mpakato) ambavyo Rais aliridhia kwaajli ya Mawakili wa Serikali.
Imeandaliwa na kutumwa kwetu na Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya AG.
22/03/2023
Post a Comment